CCM yataka wazee wenye busara kumaliza mgogoro CHADEMA

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 02:14 PM Jun 11 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla.
PICHA: MTANDAO
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakiridhishwi na mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi kufikishana mahakamani.

Imesema ushauri wao ni muda wa wazee kuwakalisha CHADEMA kuyamaliza matatizo yao ili kiendelee na shughuli zake. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, ameyasema hayo leo Juni 11, 2025,  wakati akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika jimbo la Same Mashariki, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Makalla amesema jana Mahakama Kuu imezuia shughuli za chama hicho kwa siku 14.
“Kwa sababu wanagombana wao kwa wao na sisi tunawaambia mna mgogoro, mahakama imewasikiliza waliopeleka mashtaka na imewaambia wasimame siku 14.  Baada ya uamuzi wa mahakama jana, wameanza kutafuta mchawi.
“Kwamba,’tunasikitishwa mamlaka, dola, vinahujumu chama chetu’, jamani mmepelekana mahakamani hamjapelekwa na mtu wa CCM mmepelekana wenyewe, kwa hiyo chama kinachoheshimu uhuru wa mahakama kinatakiwa kuachia na kuheshimu uamuzi wa mahakama,” amesema.
Makalla amesema wanasikitishwa na yanayotokea CHADEMA , mivutano hiyo wanafikiri ni muda wa wazee wenye busara  kuwakalisha wamalize mambo yao na huo  ndio ushauri wanawapatia ili waendelee na shughuli zao.
“Tunapenda joto lakini sasa CHADEMA imekuwa dhaifu sana, ndio kweli adui yako mwombee njaa, lakini imekuwa too much (imezidi), wache visingizio,” amesema.