Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wakazi wa jiji hilo kulinda amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, akisisitiza kuwa Dar es Salaam haiwezi kuwa eneo la majaribio katika mambo yanayohatarisha usalama wa nchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya kuzalisha umeme jijini humo, Chalamila amesema kumekuwa na vitisho vinavyoashiria uvunjifu wa amani kupitia mitandao ya kijamii na maeneo mbalimbali, jambo alilolieleza kuwa kinyume na maadili ya taifa lililojengwa katika misingi ya umoja na uzalendo.
“Tanzania ni nchi ya amani. Tuchunge misingi hiyo, tusikubali kuchochewa au kutumiwa kuvuruga utulivu tulionao. Uchaguzi ujao lazima uwe wa amani na heshima,” amesema Chalamila.
Katika ziara hiyo, Chalamila ametembelea Mradi wa Kituo cha Umeme cha Ubungo na Mradi wa Kituo Kipya cha Umeme cha Mabibo, unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 125 kutoka ndani ya nchi.
Amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zake katika kuboresha huduma ya umeme, akisema kuwa malalamiko ya kukatika kwa umeme mara kwa mara yamepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanyika.
“Katika kipindi cha nyuma wananchi walikuwa wakilalamikia kukatika kwa umeme mara kwa mara, lakini sasa hali imeboreshwa. Hizi transfoma tunazoziona zitapunguza zaidi changamoto za upatikanaji wa umeme,” ameongeza Chalamila.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya nishati ili kuhakikisha wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini wanapata umeme wa uhakika, huku akiwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kulinda amani, umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED