Dk. Mpango: Kuna uharibifu mkubwa wa ikolojia unaotishia ustawi wa utalii

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 04:10 PM Oct 16 2025
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingja akimkabidhi zawadi maalum,
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, baada ya makabidhiano ya makumbusho ya Ngorongoro-Lengai
Picha: Mpigapicha Wetu
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingja akimkabidhi zawadi maalum, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, baada ya makabidhiano ya makumbusho ya Ngorongoro-Lengai

Makamu wa Rais, Dk. Philipo Mpango, amesema kiwango cha uharibifu wa mazingira nchini ni kikubwa kiasi cha kuvuruga ikolojia na kutishia ustawi wa shughuli za utalii.

Akizungumza leo, Oktoba 16, 2025 Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, alipokwenda kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika makabidhiano ya makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai, amesema hivyo suala la utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi linapaswa kupewa kipaumbele katika uendelezaji na ukuzaji utalii.

"Kutokana na uharibifu huo tumeshuhudia mwingiliano kati ya wanyamapori na binadamu unaopelekea athari kubwa zaidi,vikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na mazao,"amesema.

Mradi wa ujenzi wa makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro/Lengai (Ngorongoro/Lengai Unesco Global Geopark), umegharimu zaidi ya Sh.bilioni 32 za Tanzania.

Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), lilitambuliwa na UNESCO na kupewa hadhi ya kuwa Jiopaki mwaka 2018.

Aidha, Dk. Mpango,amesema serikali inawakaribisha watafiti na wabobezi wa masuala ya jiolojia kutembelea makumbusho hayo, kwa lengo la kujifunza na kufanya tafiti zaidi za kiikolojia katika maeneo hayo.

Amesema mwaka 2024 Tanzania ilipokea jumla ya watalii 5,360,247 huku mapato yatokanayo na shughuli za utalii yakiongezeka kutoka Sh. milioni 700 mwaka 2020 hadi kufikia Sh.bilioni 4.0 mwaka 2024.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk.Pindi Chana, amesema kutokana na jitihada zilizofanyika katika kutunza, kuhifadhi na kuendeleza eneo la Ngorongoro, lenye urithi wa kipekee duniani na jitihada za serikali katika  kukuza ushirikiano wa diplomazia ya uchumi, mwaka 2018 serikali ya Tanzania ilipokea msaada wa kifedha kutoka serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

Balozi Dk. Chana, ameeleza zaidi kuwa fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na ujenzi wa makumbusho ya kisasa .

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas, amesema Jiopaki ya Ngorongoro/Lengai ni ya kipekee iliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyo na volkano hai, na ya pili Barani Afrika ikitanguliwa na Jiopaki ya M'Goun ya nchini Morocco.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Amos Makalla, amesema Rais, Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kufungwa kwa mradi wa taa za barabarani kuanzia Mto wa Mbu hadi katika lango la Ngorongoro ili kuchagiza shughuli za utalii katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Aidha, Makalla, amesema pia Rais Samia, ameahidi kujenga barabara ya lami ya tabaka ngumu katika eneo linaloingia hifadhi hiyo.