Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuwa endapo ataendelea kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyingine, serikali yake itahakikisha inapitisha sheria madhubuti za kulinda haki za wajane na watoto wao, ili kudhibiti wimbi la watoto wanaotelekezwa.
Akizungumza katika mkutano na jamii ya Wahindu, Waismailia, Rasta na wajane uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni, Dk. Mwinyi alisema suala hilo limepewa kipaumbele na serikali, na tayari maandalizi ya muswada wa sheria yameanza.
“Sheria hii imeanza kuandikwa, wadau wamekwishakutana na serikali imeshirikishwa. Awamu ijayo tutahakikisha sheria hiyo inakamilika na inakuwa kali dhidi ya wanaume wanaotelekeza watoto,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisisitiza kuwa lengo la sheria hiyo ni kulinda utu wa wajane na kuhakikisha watoto wote wanapata haki ya malezi, elimu na huduma bora za kijamii.
Aidha, Dk. Mwinyi alitumia nafasi hiyo kutambua mchango mkubwa wa makundi ya Ismailia na Hindu katika maendeleo ya Zanzibar, akisema ni jamii zinazojihusisha kwa uadilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Serikali inatambua mchango wenu katika kutoa huduma muhimu kama afya, elimu na maji. Ninyi ni mfano wa kuigwa kwa jinsi mnavyolea vijana kuwa raia wema na kuisaidia serikali katika maendeleo,” aliongeza.
Kwa upande wa jamii ya Rasta, Dk. Mwinyi aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwawezesha kiuchumi na kuwajengea mazingira bora ya kujiletea maendeleo.
“Tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika sekta zote, tukilenga kuinua maisha ya wananchi katika miaka mitano ijayo,” alisema.
Dk. Mwinyi alihitimisha kwa kusema kuwa dhamira yake ni kuijenga Zanzibar yenye usawa, amani na fursa sawa kwa makundi yote ya kijamii, huku serikali ikiweka mkazo katika ulinzi wa haki za watoto na wanawake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED