Dk. Mwinyi asema utalii ni sekta mama ya uchumi wa Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:50 PM Sep 22 2025
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema sekta ya utalii ni kiini cha uchumi wa Zanzibar, ambapo asilimia 30 ya mapato yote ya kisiwa yanatokana na sekta hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo, Septemba 22, 2025, wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali katika sekta ya utalii, miongoni mwao wakiwa ni watembeza watalii, wavuvi na wakulima, katika kijiji cha Nungwi, mkoani Kaskazini Unguja.

Dk. Mwinyi amesema kuwa idadi ya watalii inaongezeka kwa kasi na Zanzibar inazidi kuwa kituo kikubwa cha kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi. Kwa mwezi wa Agosti 2025, watalii 150,000 waliingia Zanzibar.

Ameongeza kuwa lengo la serikali si kuingiza watalii tu, bali kuhakikisha utalii unawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar, hasa wale wanaotoa huduma katika sekta hiyo.

 "Huo ndio utalii kwa wote, yaani kila mmoja anafanikiwa kutokana na sekta ya utalii. Serikali itahakikisha kuwajengea miundombinu inayowezesha shughuli zao kufanyika katika mazingira bora na yenye uhakika," amesema Dk. Mwinyi.