Wananchi wa Fumba, wilaya ya Magharibi B, Unguja, wameeleza masikitiko yao makubwa kuhusu kuendelea kuporwa ardhi kutokana na uwekezaji wa sekta ya utalii unaoendelea katika maeneo yao. Wamesema badala ya uwekezaji huo kuwanufaisha, umegeuka kuwa janga kwao na familia zao.
Katika kampeni ya Mgombea urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, wananchi walieleza kuwa maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa kilimo na shughuli za kijamii yamegeuzwa makazi na maeneo ya kibiashara ya wawekezaji. Hali hiyo imewafanya kukosa sehemu ya kulima na kujipatia kipato.
Wananchi walisema kilichowaumiza zaidi ni kwamba hata nafasi za ajira zinazotokana na uwekezaji huo hazijawanufaisha. Ajira hizo, kwa mujibu wao, zimekuwa zikitolewa kwa wageni wasio wakaazi wa Fumba na Bweleo, huku vijana wa eneo hilo wakibaki bila kazi na kuwa mzigo kwa familia zao.
Mama Halima Mzee, mmoja wa wananchi wa Fumba, alisema alinyang’anywa eneo kubwa la ardhi alilorithi kutoka kwa bibi zake na ambalo alikuwa akilitumia kwa kilimo. Alisema sasa ameachwa bila msaada huku akishuhudia wenye uwezo wakihodhi kila kitu.
Wananchi waliongeza kuwa maeneo muhimu ya ukanda wa bahari pia yameporwa na kupewa wawekezaji, jambo linalohatarisha maisha yao, urithi wao na hadhi ya jamii ya eneo hilo.
Kwa upande wake, mgombea urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud, alisema hajaridhishwa na hali hiyo ambayo imekuwa kilio cha mara kwa mara katika maeneo mbalimbali anayoyatembelea.
Alisema: “Wazanzibari walipaswa kuwa watu wa kwanza kunufaika na rasilimali ya ardhi, na si wageni.”
Othman aliahidi kuwa serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha wananchi wanapewa thamani kabla ya wawekezaji, akisisitiza kwamba si kila eneo lipaswe kupewa wawekezaji, bali wananchi wapewe kipaumbele na kulindwa dhidi ya unyanyasaji unaotokana na kuporwa ardhi zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED