Samia aahidi kufufua viwanda vya kubangua korosho

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:31 PM Sep 22 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kufufua viwanda vya kubangua korosho katika wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, akisema ndiyo maana serikali imeleta umeme wa kutosha katika eneo hilo.

Akizungumza leo, Septemba 22, 2025, na wananchi wa Tunduru, lenye majimbo mawili ya Kusini na Kaskazini, Samia amejinadi na kutoa ahadi hiyo huku akisisitiza kuwa Serikali yake itahakikisha maendeleo ya kiuchumi ya wilaya hiyo.

“Kuna vitalu 221 vinasubiri kutumiwa na wafugaji; baadhi vimekwisha kutumika na vingine bado tutaleta wawekezaji ili vikuze uchumi wa Wilaya hii,” amesema Samia.

Aidha, ameahidi:

  • Kumalizia barabara kwa kiwango cha lami

  • Kujenga soko la kisasa na maghala matatu ya kuhifadhia mazao

  • Kuanzisha skimu mbili za umwagiliaji maji

  • Kujenga kituo cha zana za kilimo Tunduru

  • Kununua ndege nyuki tano za kufukuzia wanyamapori wanaoingia kwenye makazi ya wananchi

  • Kuleta mpango wa kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa wilayani humo

Aidha, Samia amesema Serikali yake itachukulia kwa makini maombi ya halmashauri yaliyowasilishwa na mgombea ubunge wa eneo hilo, akiahidi kuyachakata na kuona ni yapi yatakayotekelezwa kwanza.