Ludewa waipongeza serikali, wawasilisha kero zinazowasibu

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 06:35 PM Sep 22 2025
Wananchi Ludewa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wananchi Ludewa.

Wakazi wa Ludewa mkoani Njombe wameipongeza serikali kwa ujenzi wa Daraja la Songea- Ludewa, huku wakiiomba kumaliza ujenzi wa Barabara ya Lusitu-Mndindi kwa kiwango la lami.

Wakizungumza na Nipashe leo Septemba 22 katika Uwanja wa Halmashauri ya Ludewa, wakazi hao walisema katika miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan wameletewa miradi mingi ya maendeleo lakini bado wanasumbuliwa na tatizo la ukosefu wa maji na ubovu wa barabara.

Chesco Kilamba kutoka Kijiji cha Mndindi wilayani Ludewa mkoani Njombe anasema eneo wanaloishi wanakasumbuliwa na maji.

Anasema: " Tunampongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyotufanyia wakazi wa Mndindi, tunamhakikishia kura za kutosha Oktoba, lakini akiendelea madarakani atutarulie tatizo la ukosefu wa maji. Maji yanatoka mara moja kwa wiki".

Anasema umeme unapatikana kwa wingi, lakini upatikanaji wa maji bado ni tatizo.

Prisca Mlelwa kutoka Mtaa wa Kiombo Ludewa Mjini anasema: " Barabara ya Lusitu- Mtindi ni vumbi sana. Nyakati za mvua haipitiki. Tunaiomba serikali imalizie ujenzi wake".

Josen Komba kutoka Ludewa Mjini anaishukuru serikali kwa kujenga Daraja la Songea pamoja na upatikanaji wa mbolea kwa wakati.

Anasema mbolea inapatikana kwa wakati lakini changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni wakati wa uuzaji wa mahindi.