Wadau mbalimbali wamekutana jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili na kuongeza uelewa wa umma kuhusu usalama barabarani, hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Kikao hicho kilishirikisha wataalam wa usanifu, ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na wanafunzi kutoka shule za msingi Pius Msekwa, Kunduchi na Tegeta, ambazo zipo kando ya barabara kuu na zinatarajiwa kunufaika na Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2).
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo, amesema lengo la majadiliano hayo lilikuwa ni kusikiliza maoni na uzoefu wa wanafunzi kuhusu safari zao za kila siku kwenda na kurudi shuleni.
“Mpango huu unaangazia umuhimu wa kushughulikia mahitaji ya watumiaji wa barabara walio hatarini, hasa watoto, kwa kuwa wako kwenye hatari kubwa. Tunataka kuondokana na mtazamo wa kuyapa kipaumbele magari pekee na badala yake kuzingatia usalama wa binadamu, hususan watoto,” amesema Kalolo.
Mradi wa DMDP 2, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya dola milioni 330, unatarajiwa kuboresha takriban kilomita 260 za barabara kati ya mwaka 2025 na 2030.
Kalolo amebainisha kuwa mpango huo unalenga pia kuanzisha jukwaa litakalowawezesha watoto kubadilishana uzoefu wao na viongozi pamoja na wahandisi wanaohusika katika miradi ya barabara.
“Kwa kujumuisha mawazo ya watoto katika kubuni miundombinu, tunaweza kujenga barabara salama zaidi kwa watembea kwa miguu na watu wenye mahitaji maalumu. Hii inaweza kusaidia kuzuia vifo na majeraha kwa watoto,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa mpango huo unaungwa mkono na serikali, hususan TARURA na Benki ya Dunia, na kwamba taasisi yake itatumia vyombo vya habari kuongeza uelewa wa usalama barabarani unaozingatia watoto kwa watunga sera, wataalamu na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Agatha Tembo kutoka mradi wa DMDP-KMC, amesema ushirikiano wa wadau wote ni muhimu katika kuimarisha usalama barabarani, na alisisitiza wajenzi kuweka alama na vibao vya mbao vya tahadhari kwa uangalizi maalum, ili visichukuliwe na wakazi kwa matumizi ya nyumbani.
Naye mwalimu wa Shule ya Msingi Kunduchi, Prosper Lyimo, ameshauri walimu kuwa na utaratibu wa kuwakumbusha wanafunzi kila siku asubuhi na baada ya masomo kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza barabarani na kuwasisitiza kuwa makini wakati wa ujenzi na matumizi ya barabara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED