“Serikali Kuu imekuwa ikipiga fedha kupitia miradi ya maendeleo” – Jussa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:23 PM Sep 22 2025
Meneja wa Kampeni wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa Kampeni wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa.

“Ni aibu kubwa. Wakati mfuko wa saruji ulikuwa shilingi 17,000, wao waliweka hesabu ya shilingi 23,000. Hii ni dhulma kwa wananchi na wizi wa wazi katika masoko yote ya Unguja na Pemba,” alisema Meneja wa Kampeni wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa, jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Tomondo, nje ya mji wa Zanzibar.

Kauli hiyo ilizua hamasa kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza Jussa pamoja na Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Othman Masoud Othman.

Jussa alifichua pia kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vya SMZ vimekuwa vikibebeshwa majukumu yasiyokuwa yao kwa maslahi ya kisiasa, akisema hutumika kama kivuli cha makampuni binafsi kutoka Dar es Salaam.

“Askari wetu wamelazimishwa kufanya kazi za nguvu wakati wachache wakiendeleza maslahi binafsi. Hii ni dharau kwa wananchi na matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na usalama,” aliongeza Jussa.

Kwa upande wake, mgombea urais wa chama hicho, Othman Masoud Othman, aliwaahidi wananchi kwamba serikali ya ACT Wazalendo italinda mali za umma, kurejesha heshima ya vikosi vya SMZ na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inawanufaisha wananchi moja kwa moja.

1