Wananchi Zanzibar wafurahia ahadi ya Mfuko wa Zaka wa ACT Wazalendo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:26 PM Sep 22 2025
Wananchi Zanzibar wafurahia ahadi ya Mfuko wa Zaka wa ACT Wazalendo.
Picha:ACT
Wananchi Zanzibar wafurahia ahadi ya Mfuko wa Zaka wa ACT Wazalendo.

Siku moja baada ya Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kuahidi kuanzisha mfumo maalumu wa Zaka kwa ajili ya kuwasaidia maskini na mafukara wa Zanzibar, wananchi wamepokea pendekezo hilo kwa furaha kubwa, wakiliona kama suluhisho la muda mrefu kwa umasikini unaoikabili jamii.

Kwa muda mrefu, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na changamoto za maisha duni na kipato cha chini, hali iliyowaathiri maelfu ya familia. Wananchi wanaamini kuwa mfuko huo wa Zaka utatoa mwanga mpya wa matumaini na nafasi ya kujikwamua kiuchumi.

Wananchi wazungumza
Ali Machano Makame, mkazi wa Paje, alisema hali ya maisha imekuwa ngumu na kwamba ahadi ya kuanzishwa kwa mfuko huo italeta matumaini mapya kwa familia zisizojiweza.

 “Hii ni nafasi ya kujipanga upya kiuchumi na kusaidia wale wasio na uwezo kupata matumaini ya maisha bora,” alisema Machano.

Maryam Ismail wa Shakani, Unguja, alisema mara nyingi hukosa hata chakula kutokana na ugumu wa maisha. Anaamini mfuko wa Zaka utawasaidia kupata mitaji midogo ya kibiashara.

 Aliongeza kuwa tofauti na mikopo iliyoahidiwa na serikali iliyopo madarakani, ambayo haijawahi kuwafikia licha ya kusubiri kwa miaka mitano, mfuko huu unaweza kuwa wa kweli na wenye tija.

Ahadi ya Othman Masoud
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara mkoani Kaskazini Unguja jana, Othman Masoud alisema Zanzibar inahitaji mabadiliko ya kweli, ikiwemo kuwasaidia wananchi wanyonge.

 Aliahidi kwamba ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi wake, ataweka rasmi mfuko wa Zaka utakaosimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji.

 “Wazanzibari wanahitaji kiongozi mwadilifu na mkweli. Mimi sijawahi kuhusishwa na ufisadi, na ndiyo maana nasema hili linawezekana. Nipeni kura zenu ili tufanikishe mabadiliko haya,” alisema Othman.

Ufisadi wakosolewa
Mgombea huyo alilaani vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kutawala serikali ya sasa, akisema Zanzibar ni nchi yenye neema lakini rasilimali zake zimekuwa zikiporwa.

 Alibainisha kuwa miradi ya maendeleo imegeuzwa njia ya kupiga mabilioni ya fedha huku wananchi wakiendelea kuishi maisha magumu.

 Alikumbusha kuwa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionesha wazi ufisadi kila mwaka, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.

 “Hebu jiulizeni, ni wangapi walifikishwa mahakamani baada ya ripoti ya CAG? Ni kipi kilichofanyika hadi leo? Ndiyo maana tunasema hawa wote ni mafisadi na lao ni moja,” alisisitiza.

Wananchi wahamasika
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walisisitiza kuwa ahadi ya mfuko wa Zaka imewapa hamasa kubwa kushiriki katika uchaguzi ujao, wakiamini ACT Wazalendo ndicho chama pekee kinachoweza kuleta mabadiliko ya kweli Zanzibar.