WATOTO wanaoishi nje ya familia, wanakoseshwa malezi bora, ikiwamo kutotambua asili ya tamaduni za makabila yao, wengine hujikuta wakibadilishwa imani za dini za awali.
Hayo yameibuliwa kwenye mjadala huo ulihusu Mkataba wa Kimataifa wa kubadilisha malezi ya watoto, ulioandaliwa na Serikali ya Uingereza, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali duniani, unaosisitiza watoto kulelewa ndani ya familia badala ya vituo vya yatima. Rose Kagoro kutoka Railway Children anasema:
Siyo ajabu kukuta mtoto aliyezaliwa kwenye familia ya Kiislamu akilelewa kwenye kituo cha Kikristo na baadaye akabadilisha dini yake ya asili. Vivyo hivyo, mtoto wa Kikristo akilelewa kwenye kituo cha Kiislamu naye anabadilishwa dini yake ya awali.”alisema Kagoro.
Wadau hao wamesisitizwa kujenga uelewa wa mkataba huo na kuchunguza uwezekano wa Tanzania kuuridhia, ili kusaidia kupunguza idadi ya watoto wanaolelewa nje ya familia, hususan katika vituo vya kulelea yatima.
Aidha jamii imehimizwa ielekeze misaada moja kwa moja kwenye familia zenye kipato duni, badala ya kupeleka misaada yote vituoni, hali inayochochea baadhi ya watoto kutoka familia masikini kukimbilia vituo, ambapo wengine hukumbana na ukatili, ikiwemo wa kingono.
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Asha Mbaruku, alisema mtoto anapokosa malezi ya kifamilia anakumbana na changamoto kubwa za kimaadili, hivyo serikali inasisitiza kipaumbele cha malezi ya kifamilia.
Anatoa wito kwa watu wenye moyo wa upendo kuasili watoto kwa kufuata taratibu zilizowekwa:
“Utaratibu wa kuasili mtoto ni wa kisheria na unaolenga usalama wake. Wengine huona ni kero, kumbe hata kuzaa ni mchakato wa miezi tisa, hivyo malezi lazima pia yaheshimiwe kama mchakato.”
Mratibu Mwandamizi wa Malezi Mbadala kutoka SOS Tanzania, Abasi Makalanga, anasema tayari wameanza mchakato wa kuwaondoa watoto kwenye vituo na kuwakabidhi kwa familia mbadala.
Anabainisha kuwa Dar es Salaam waliokuwa watoto 130 wamepungua hadi 57, Zanzibar kutoka 100 wamebaki 4, Mwanza kutoka 120 wamebaki 76 na Arusha kutoka 144 hadi 54.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED