Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na wakazi wa Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kuwaahidi mageuzi makubwa katika sekta ya utalii. Amesema serikali yake itaweka mazingira rafiki ya biashara kwa kuanzisha maeneo rasmi ya kuuza bidhaa za kiasili na kazi za mikono karibu na vivutio vya utalii ili wananchi wanufaike moja kwa moja.
Katika juhudi za kuimarisha uchumi wa wananchi, Dk. Mwinyi ameahidi kuwa serikali itatoa mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali wa sekta ya utalii. Aidha, ameongeza kuwa pamoja na mikopo hiyo, serikali itaratibu mafunzo ya ujasiriamali ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri na kusaidia kuongeza mnyororo wa thamani katika bidhaa na huduma zinazotolewa.
Vilevile, Dk. Mwinyi amesema serikali itashughulikia changamoto za mikataba isiyo na uwazi kati ya wawekezaji na wananchi ili kulinda haki za wakazi wa maeneo ya utalii. Amesisitiza kuwa wawekezaji watahimizwa kuzingatia maslahi ya jamii inayowazunguka, huku serikali ikihakikisha mazingira salama kwa uwekezaji.
Akitamatisha hotuba yake, Dk. Mwinyi amesema CCM hutoa ahadi zenye kutekelezeka na sio maneno matupu ya kampeni. Alisisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020 ni ushahidi kuwa ahadi zinazotolewa sasa pia zitatekelezwa kwa vitendo pindi atakapochaguliwa tena.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED