Dk. Mwinyi awataka Wazanzibari kudumisha amani

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 05:43 PM Sep 22 2025
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendeleza amani, mshikamano na maridhiano nchini, akisisitiza kuwa yeyote atakayevunja amani atadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shangani Mkokotoni, jimbo la Kijini, mkoani Kaskazini Unguja.

Akizungumzia sekta ya afya, Dk. Mwinyi amesema serikali yake imeimarisha huduma hiyo kwa kiasi kikubwa, ambapo huduma zote za afya pamoja na chakula cha milo mitatu kwa wagonjwa wanaolazwa hospitalini hutolewa bure.

 “Huduma zetu zimeimarika kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wanapopata nafuu na kuruhusiwa, wanakataa kutoka hospitalini kutokana na huduma nzuri wanazopata,” amesema Dk. Mwinyi.

Aidha, ameahidi kuendeleza miradi ya ujenzi wa barabara mijini na vijijini ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na usafirishaji kwa wananchi, akibainisha kuwa miundombinu bora ni chachu ya maendeleo ya Zanzibar.