Dk. Mwinyi: Serikali imefanikiwa kuondoa ubaguzi na siasa za chuki

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 09:59 AM Oct 06 2025
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa ubaguzi, mifarakano na siasa za chuki katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema umoja wa Wazanzibari ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya Serikali na maendeleo ya Taifa, huku akisisitiza kuwa kigezo cha utoaji wa nafasi za uongozi ni uwezo wa mtu, siyo asili au anatoka wapi.

“Serikali chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi imefanikiwa kuondoa ubaguzi na kuimarisha maridhiano pamoja na umoja wa kitaifa kwa maslahi ya wananchi wote,” alisema Dk. Mwinyi.

Kauli hiyo aliitoa Oktoba 5, 2025, alipokutana na viongozi wa dini, wakiwemo masheikh, watawa (masista) na mapadri, katika ukumbi wa mikutano wa Skuli ya Utaani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa kampeni zake na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya jamii.