Dk. Tindwa ataja sababu Samia kuchaguliwa tena

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:10 PM Oct 16 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dk. Chakou Tindwa.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dk. Chakou Tindwa, amesema uzoefu kwenye uongozi alionao mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho Dk. Samia Suluhu Hassan, ni sababu mojawapo ya kumfanya aendelee kuiongoza Tanzania kwa miaka mingine Mitano.

Dk. Tindwa ameyasema hayo leo wilayani Mafia mkoani Pwani wakati wa mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani humo kwa lengo la kukumbushana masuala muhimu, kuelekea Uchaguzi Mkuu, ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

“Rais Samia anapaswa kupewa tena ridhaa ya kuongoza kwa sababu ni kiongozi mwenye uzoefu, amewahi kuwa mbunge, waziri, na Makamu wa Rais. Lakini Dk Emmanuel Nchimbi ameanzia uongozi tangu akiwa chipukizi hivyo ni viongozi wenye sifa ya kulipeleka taifa letu mbele,” amesema Dk. Tindwa.

Kadhalika, Dk. Tindwa amesema serikali chini ya Rais Samia imefanya kazi kwa vitendo ikiwemo kukamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati.

“Kwa sasa nchi inaweza kufikisha dawa katika hospitali mbalimbali, ujenzi wa miundombinu na miradi imetekelezwa ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, na Daraja la Kigongo Busisi miradi ambayo ambayo iliachwa na mtangulizi wake hayati John Magufuli na yote imekamilishwa,” amesema.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mafia Amina Khatibu
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mafia Amina Khatibu, amesema, tayari umoja wao umeshajiandaa kuhakikisha mgombea wa chama chao Dk. Samia anapata urais ili aendelee kufanikisha miradi mbalimbali yenye tija kwa vijana.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mafia Mohamed Faki, amebainisha namna miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia ulivyoibadilisha wilaya hiyo kimaendeleo.

“Tangu Rais Dk. Samia aingine madarakani ametoa zaidi ya Sh. Bilioni 60 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humu ikiwemo ujenzi wa barabara, madarasa, upatikanaji wa maji na huduma za afya,” amesema Faki.