Dk.Samia: Nitamaliza kero ya maji Misungwi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:22 PM Oct 07 2025
Dk.Samia: Nitamaliza kero ya maji Misungwi

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake katika miaka mitano ijayo itamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Dk Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Oktoba 7, 2025 alipokuwa wilayani Misungwi mkoani Mwanza, katika mkutano wake wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Ameeleza anatambua changamoto inayowakabili wananchi wa eneo hilo ni maji, lakini tayari Sh888 bilioni zimetolewa kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa maji wa kilomita 38 wilayani humo.

Ameeleza matenki mawili yenye ujazo wa lita 150,000 na lita 90,000 yamejengwa Misungwi na Igokelo ili kupeleka maji Mbela, Mwambola, Ng’ombe, Iteja na Mwamanga na tayari umefikia asilimia 87.

Amesema mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wananchi 22,482.

Ameeleza miradi 10 yenye thamani ya Sh65 bilioni inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa Ukiliguru unaohudumia vijiji 19 vya Kata za Usagara, Ukiliguru na Olamije.

“Mradi huu utanufaisha wananchi 85,500, pia tuna mradi mwingine wa Ilujamate mpaka Buhingo, unaotarajia kuhudumia vijiji 16,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Samia, hatua hizo ni uthibitisho wa dhamira ya CCM kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama.