Dongobesh yarejesha tabasamu huduma ya maji

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:57 AM Oct 16 2025
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simendu (katikati), akizundua kisima cha maji Dongobesh.
Picha: Godfrey Mushi
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simendu (katikati), akizundua kisima cha maji Dongobesh.

Taasisi ya Bridge Of Hope ya Ujerumani, imerejesha tabasamu kwa wanafunzi zaidi ya 2,000 wa Dongobesh, Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, baada ya kuchimba kusima kirefu cha majisafi ili kumaliza tatizo la kusotea huduma hiyo katika vijiji vya jirani.

Wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi za Mchepuo wa Kiingereza ya Msingi ya Lea na Sekondari ya Dongobesh, walikuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji wakati wa masomo, huku wakazi wao wakihemea maji machafu kwa ajili ya matumizi ya majumbani.

Mwasisi wa taasisi hiyo, Arnd Weil akizungumza jana, Wilayani hapa, wakati wa uzinduzi wa kisima kirefu cna maji kilichogharimu Sh.milioni 100, amesema wameguswa kutatua changamoto hiyo ya upatikanaji wa maji, ili kuongeza chachu ya maendeleo kwa jamii.

Aidha, amesema wanafunzi na wananchi hao wameanza kunufaika na huduma hiyo ya majisafi, ambapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufata huduma hiyo, huku baadhi ya wanafunzi wakikatisha ratiba za masomo yao ili kupata maji ya kunywa na matumizi mengineyo.

Raia huyo wa Ujerumani, amesema wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Dongobesh, ndio waliolengwa zaidi na mradi huo, baada ya kupitia changamoto za kiafya.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Simendu, baada ya kuzindua mradi huo, ameishukuru taasisi hiyo, huku akisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuwahudumia wananchi ili kuongeza tija kwa jamii na kuwapa fursa ya kujikita katika shughuli za uzalishaji mali.

Naye, Mwasisi Mwenza wa Taasisi ya Bridge of Hope, Simone Weil, amesema taasisi hiyo iliguswa kutoa  ufadhili huo wa kuwachimbia kisima wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Msingi ya Lea iliyoko Dongobesh.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Anna Paul, ameeleza furaha yao baada ya kuwa na uhakika wa huduma ya majisafi shuleni hapo,akisema ahueni hiyo imewafuta machozi hasa wasichana waliokuwa wakipata changamoto ya kukosa maji wakati wa hedhi.

Wafadhili na waasisi wa Taasisi ya Bridge of Hope, wakifuatilia wasanii wa ngoma za asili waliokuwa wakitumbuiza (hawapo pichani), wakati wa uzinduzi wa kisima cha maji Dongobesh.