MKUU wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, Rachel Kassanda, ametoa tahadhari kwa wananchi wote wa wilaya hiyo kuchukua hatua baada ya kuibuka ugonjwa wa kichwa cha mbwa ambao umeripotiwa kuathiri baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya jamii robo ya nne, Kassanda alisema kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kutoka kwa wataalamu za afya wa wilaya hiyo kuibuka kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa katika baadhi ya vijiji na kata hali inayosababisha hatari kwa wananchi.
Alisema kuanzia sasa tahadhari kwa wananchi wote ichukuliwe kuepuka kung'atwa na wanyama hao na pale inapotokea kuwahi haraka kwenda kupata huduma za matibabu kwenye vituo vya kutolewa huduma ikiwamo hospitali.
Aidha, maeneo ya vijijini na mijini kumekuwa na mbwa wanaoonesha tabia zisizo za kawaida, ikiwamo ukali kupita kiasi, kukimbia bila mwelekeo na kushambulia watu bila sababu.
“Tumeanza kupokea taarifa za visa vya watu kung’atwa na mbwa, baadhi yao tayari wamepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu ya awali, hili ni jambo la dharura linalohitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu. Ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni hatari na unaweza kusababisha kifo kama hautatibiwa kwa wakati,” alisema Kassanda.
Alisema ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni hatari kwa binadamu na kwa mujibu wa wataalamu wa afya gharama za matibabu kwa mtu aliyeathirika na ugonjwa huo ni kubwa.
Alizitaka familia zote zinazomiliki mbwa kuwapeleka kwa wataalam wa mifugo kwa ajili ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo, na kuwaonya wananchi wanaowaficha mbwa wanaoonesha dalili za ugonjwa.
Katika hatua nyingine, ameiagiza Idara ya Mifugo ya halmashauri kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji ili chanjo kwa mbwa wote ianze huku akisisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na kuchukua hatua wanapong’atwa na mbwa.
"Tunaomba wananchi watoe ushirikiano, wasiwafiche mbwa wanaoumwa, na pia wawapeleke kwa wataalam mara moja pindi wanapoona tabia zisizo za kawaida. Watoto pia waelimishwe kuepuka kucheza au kukaribia mbwa wanaotembea ovyo mitaani,” aliongeza.
Mkuu huyo wa wilaya pia alitoa wito kwa wamiliki wa mbwa kuepuka kuwaachia wanyama hao kuzurura mitaani bila uangalizi, ni kinyume cha sheria na kunaweza kuhatarisha maisha ya watu wengine.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Ruben Mwakilima, amekiri kuwapo kwa ugonjwa huo na kueleza tayari baadhi ya watu wamegundulika na ugonjwa huo na kufanyia matibabu ya haraka.
Kaimu Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Laurent Simba, ameeleza kuwa idadi kubwa ya mbwa wanaomilikiwa na wananchi, huku baadhi yao wakikosa chanjo muhimu za kinga. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya na mifugo imeahidi kuweka mkakati wa muda mfupi na mrefu kuhakikisha ugonjwa huo unakomeshwa na jamii inalindwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED