SHIRIKA la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), limepewa cheti cha pongezi na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kwa kutambua mchango wao wa kuibua mabinti na wasichana wanaotoka katika mazingira magumu, kuwasomesha na kuwapatia vifaa kazi bure.
Mabinti hao wameibuliwa kupitia mradi wa “Haki yangu Chaguo langu” unaotekelezwa katika mikoa ya Shinyanga na Mara, kwa kushirikiana na UNFPA kwa ufadhili wa serikali ya Finland na wanaofikiwa ni wale wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24.
Akikabidhi cheti hicho leo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika hilo, Aneth Mushi, amesema cheti hicho kikawe chachu ya kuwaibua wasichana wengine, ili kuendelea kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye jamii na familia zao.
Amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana kwa karibu na serikali kupitia ofisi ya maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika kuwaibua mabinti na wasichana, wanaotoka katika mazingira magumu na waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Niwapongeze WiLDAF kwa hatua ya kuwaibua mabinti na kuwapatia ujuzi ambao unakwenda kuwasaidia katika maisha yao na kuondokana na utegemezi kwenye familia zao, wapo waliokatisha masomo yao kwa vitendo vya ukatili, ikiwamo ndoa na mimba za utotoni na sasa wameibukia kwenye fani za ufundi stadi,” ameongeza.
Amesema, licha ya masomo hayo pia waliwapatia elimu ya afya ya uzazi, ili kutokupata maambuzi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kuwataka kuwa wamoja katika vikundi, ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri na sio kuingia kwenye mikopo umiza inayoshusha uchumi wao.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Kahama, Swaiba Chemchem, amesema watahakikisha wanawaunganisha kwenye vikundi vya ujasirimali kulinganisha na ujuzi wao waliosoma na kuhakikisha wanapata mikopo itayowawezesha kupata mikopo ya kuanzisha sehemu za kufanyia kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED