Historia fupi ya Job Yustino Ndugai katika uongozi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:36 PM Aug 06 2025
Job Yustino Ndugai
Picha: Mtandao
Job Yustino Ndugai

Aliyewahi kuwa Spika na Mbunge wa Kongwa, Job Yustino Ndugai amefariki Dunia, leo Agosti 6, 2025, taarifa ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dk. Tulia Ackson imeeleza kuwa msiba umetokea Dodoma.

Dk. Tulia amesema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya Marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Historia Fupi ya Job Yustino Ndugai Katika Siasa hadi Ushindi wake kwenye Kura za Maoni 2025

Job Yustino Ndugai ni mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amehudumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali za uongozi wa kisiasa na kitaasisi nchini Tanzania. Alizaliwa mwaka 1963 na alianza safari yake ya kisiasa kwa mafanikio makubwa yaliyotanguliwa na elimu ya juu yenye mwelekeo wa usimamizi na uongozi.

Elimu na Maandalizi ya Uongozi

Ndugai alipata Stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Chuo cha Mweka kati ya mwaka 1986–1988, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata Shahada ya Kwanza (1989–1993). Aliendelea na masomo ya juu nchini Norway katika Chuo cha Kilimo, akihitimu Post Graduate Diploma (1994–1995) na Shahada ya Umahiri (1995–1996). Baadaye, alisoma Shahada ya Umahiri katika Usimamizi wa Biashara (MBA) kupitia taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) kati ya mwaka 2005–2008.

Safari ya Kisiasa

Job Ndugai alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa mwaka 2000, nafasi aliyoendelea kushinda katika chaguzi zilizofuata kutokana na uaminifu wa wananchi na uwezo wake wa kiuongozi. Mwaka 2010, aliteuliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge, akihudumu hadi mwaka 2015.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa alioutekeleza kwa miaka sita hadi Januari 2022 alipojiuzulu. Akiwa Spika, Ndugai alijijengea sifa ya kuwa mtetezi wa heshima ya Bunge, msimamo wake juu ya matumizi ya fedha za umma na suala la madeni ya taifa uliwahi kuzua mijadala mikali ya kisiasa, na hatimaye kupelekea kujiuzulu kwake.

Kazi Nje ya Siasa

Kabla na hata wakati wa maisha yake ya kisiasa, Ndugai aliwahi kufanya kazi katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Pori la Akiba la Selous, na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). Aidha, ni mwalimu kitaaluma na amepitia mafunzo mbalimbali ya kijeshi na kiutawala ndani na nje ya nchi.

Kura za Maoni 2025

Licha ya kujiuzulu nafasi ya Spika, Job Ndugai ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa katika Jimbo lake. Katika kura za maoni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, Ndugai ameibuka mshindi kwa kishindo kwa kura 5690, jambo lililodhihirisha bado anayo imani kubwa kutoka kwa wananchi wa Kongwa pamoja na wanachama wa chama chake.

BARUA.png 807.74 KB