Waajiri wapigwa msasa ulipaji mafao kwa wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:00 PM Aug 06 2025
Meneja wa PSSSF kanda ya Ilala, Amina Kassim.
Picha;Mpigapicha Wetu
Meneja wa PSSSF kanda ya Ilala, Amina Kassim.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) umeendesha semina kwa waajiri wa Mkoa wa Dar es salaam wanaoshughulikia masuala ya wanachama wa PSSSF kwa lengo la kuwajengea uweze maafisa hao juu ya masuala mbalimbali ya mfuko.

Akifungua mafunzo hayo ambayo yamehudhuriwa na washriki kutoka taasisi 159, Meneja wa PSSSF kanda ya Ilala, Amina Kassim amesema, “Mpango huu wa mafunzo ni mpango endelevu wa Mfuko kwani semina kama hizi huwa zinatolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ya mfuko ikiwemo huduma na bidhaa mpya, lakini la msingi zaidi ni kupata mrejesho kutoka kwa wanachama wetu kupitia kwenu wataalamu wa kada ya utumishi.” amesema.

Amesema semina hiyo inafanyika ambapo PSSSF imetimiza miaka saba tangu kunzishwa kwake, kwani PSSSF ilizaliwa Agosti 1, 2018 kupitia sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ya mwaka 2018.

“Tunawaambia wanachama wetu, waendelee kufurahia huduma zetu. Mfuko sasa unalipa pensheni kila ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi. Malipo ya mkupuo baada ya mtumishi kustaafu yanalipwa kwa wakati kama sheria inavyoelekeza.” amefafanua Amina.

Meneja huyo wa kanda ya Ilala alisema, mafanikio ya PSSSF yanatokana na uongozi makini wa serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambao umehakikisha unalipa michango ya watumishi kila mwenzi, kwa hakiki jambo hili ni la kujivunia kwani linaendeleza uimara wa mfuko wa kuweza kulipa mafao kwa wakati kwa wastaafu na wanufaika wengine.

Katika semina hiyo mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na; Kazi na majukumu ya PSSSF, Mafao ya kifo na pensheni ya miezi 36, Uhuishaji pensheni, GePG na uandikishwaji kupitia PSSSF portal, Home mortgage na Maadalizi ya kustaafu.