TARURA yajenga madaraja 439 kwa teknolojia ya mawe

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 09:29 AM Aug 07 2025
Afisa Habari Mwandamizi TARURA Raphael Kilapilo
Picha: Pilly Kigome
Afisa Habari Mwandamizi TARURA Raphael Kilapilo

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umefanikiwa kujenga madaraja 439 kwa kutumia teknolojia ya mawe na matofali ya kuchoma, hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ujenzi na kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 75.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Mratibu wa Ujenzi wa Madaraja na Barabara za Mawe kutoka TARURA, Mhandisi Mshauri Fares Ngeleja, amesema kuwa ujenzi huo umetumia Shilingi bilioni 15 pekee, tofauti na gharama ya zaidi ya bilioni 90 ambayo ingewatumika endapo wangetumia teknolojia ya kawaida ya saruji na tofali.

“Tumeweza kutumia teknolojia rahisi, salama na rafiki kwa mazingira ambayo imetuwezesha kuunganisha vijiji na miji kwa ufanisi mkubwa, na pia kuboresha huduma za kijamii kama vile afya, elimu, masoko, na maeneo ya ibada,” alisema Mhandisi Ngeleja.

Ameongeza kuwa teknolojia hiyo pia imeleta manufaa ya kimazingira kwa kupunguza uharibifu wa ardhi na vyanzo vya maji, kwani haitegemei matumizi makubwa ya vifaa vinavyotokana na viwanda vinavyotoa hewa chafu.

“Tumeweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ufanisi wa usafirishaji, hasa nyakati za mvua ambapo zamani wananchi walikuwa wakikwama kuvuka,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Ngeleja, miundombinu hiyo pia imesaidia kurahisisha ushiriki wa wakulima, wavuvi na wafugaji kutoka pembezoni mwa miji kufika katika maeneo muhimu kama maonyesho ya Nane Nane, masoko na vituo vya huduma kwa wakati.

Kwa upande wake, Afisa Habari Mwandamizi wa TARURA kupitia Mradi wa Maendeleo ya Miji (DMDP), Raphael Kilapilo, aliwataka wananchi kutumia vizuri miundombinu hiyo kwa kuilinda dhidi ya uharibifu.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuitunza miundombinu ya barabara na madaraja kwa sababu hiyo ni dira ya maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo. TARURA itaendelea kuhakikisha changamoto za muda mrefu zinafanyiwa kazi kwa ufanisi na ubora unaostahili,” alisema Kilapilo.

TARURA imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya jamii kwa kuimarisha miundombinu ya barabara vijijini na mijini, hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi, kijamii na huduma za msingi kufikika kwa urahisi.

IMG-20250807-WA0071.jpg 79.94 KB