Jeshi la Polisi lawashikilia watu uharifu kura za maoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:11 PM Aug 08 2025
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Simon Maigwa
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Simon Maigwa

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika na jaribio la kufanya uhalifu wakati wa zoezi la upigaji kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Vunjo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Simon Maigwa, watu hao walikamatwa usiku wa kuamkia Agosti 4, 2025, wakiwa na silaha za jadi, mabomu na kamba ngumu, na wanadaiwa kumjeruhi kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Safina, ambaye aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Himo.

Kamanda Maigwa amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wote waliopanga njama hizo, huku akithibitisha kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni mtu mwenye uhusiano wa karibu na mmoja wa wagombea wa nafasi ya ubunge kupitia CCM katika uchaguzi huo wa kura za maoni.

"Jeshi linaendelea kuchunguza taarifa hizi kwa kina, zikiwemo zile zinazomhusisha mmoja wa waliokuwa wagombea wa ubunge kuhusika na kikundi hicho kilichokusudia kuvuruga mchakato wa uchaguzi," alisema Kamanda Maigwa.

Hata hivyo, alikataa kuweka wazi majina ya wahusika kwa sasa kwa sababu za kiuchunguzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema suala hilo linapaswa kuelekezwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho ngazi ya mkoa, ambaye pia ni Katibu wa CCM mkoa.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya chama zinaeleza kuwa tukio hilo la vurugu liliratibiwa kwa ukaribu na mmoja wa wagombea ambaye anatuhumiwa kuwa na mahusiano ya kindugu na mmoja wa waliokamatwa na Polisi.

Katika uchaguzi huo wa kura za maoni uliohusisha wagombea sita, Enock Koola aliibuka mshindi baada ya kupata kura 1,999, akiwapiku Dkt. Charles Kimei (861), Yuvenal Shirima (659), Didas Lyamuya (329), Prosper Tesha (177), na Delfina Kessy aliyepata kura 29 pekee.