Watoto wawili wamefariki dunia na bibi yao kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua iliyoambatana na upepo mkali na radi iliyonyesha jana katika Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza leo, tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:30 mchana, Agosti 7, 2025, katika mtaa wa Bulola "A", Kata ya Buswelu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea wakati Grace Kateti (52), ambaye ni bibi wa watoto hao, alipokuwa akipika chakula cha mchana chini ya mti uliopo jirani na nyumba yao.
Watoto waliopoteza maisha wametambulika kuwa ni Mwasi Michael (11), mwanafunzi wa darasa la tano, na Charles Michael (6), mwanafunzi wa darasa la pili — wote wakiwa wanasoma katika Shule ya Msingi Bulola.
Bibi yao, Grace Kateti, ambaye alipigwa na radi hiyo pamoja na wajukuu zake, alipata majeraha na kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Buzuruga, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure kwa uchunguzi zaidi.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua zinazoambatana na upepo mkali na radi, kwa kuepuka kukaa maeneo ya wazi au chini ya miti, ili kujiepusha na madhara kama hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED