CUF yapitisha majina wagombea urais, yafukuza wanachama saba

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:49 PM Aug 08 2025
CUF yapitisha majina wagombea urais, yafukuza wanachama saba

Chama Cha Wananchi (CUF) kimepitisha majina ya wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku kikiwaondoa wanachama saba waliodaiwa kufanya vurugu na kukwamisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama kilichofanyika Agosti 8,2025, amewataja wagombea wa urais wa Tanzania Bara ni Nkunyuntila Siwale na Gombo Samandito, wakati upande wa Zanzibar ni Mhandisi Habib Mohamed Mnyaa, Mhandisi Hamad Masoud Hamad na Dk. Mohamed Khatib Mikidadi. Majina hayo yatapigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu Maalum utakaofanyika Agosti 9, 2025.

Prof. Lipumba amesema wanachama saba waliotajwa kuongoza vurugu na kupinga kusaini mahudhurio wamefukuzwa uanachama kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Waliofukuzwa ni Dauda Hassan Kasigwa, Yasin Mrotwa, Abdallah Dadi Ubwa, Faki Suleiman Mohamed, Rashid Ali Hamad, Mohammed Nassor Hamad na Yusuf Ali Mussa.

Amesisitiza kuwa chama kimejipanga kushinda uchaguzi mkuu na kushughulikia changamoto za uchumi, ajira, gharama za maisha na ufisadi.