Maonesho ya Kilimo Nanenane Kanda ya Mashariki yamemalizika leo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mkoani Morogoro, kwa mafanikio makubwa, huku yakionesha teknolojia za kisasa katika kilimo, ufugaji, uvuvi na usindikaji wa mazao.
Miongoni mwa mambo yaliyovutia ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji kwa teknolojia ya kisasa, ufugaji wenye tija, uvuvi wa kisasa pamoja na uchakataji wa mazao kwa viwango vya kimataifa vinavyoongeza thamani na ushindani sokoni.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, amesema mabadiliko makubwa yanayoonekana ni matokeo ya uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuboresha sekta ya kilimo.
“Kauli mbiu ya mwaka huu — ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025’ — ni somo la wazi kuwa maendeleo ya sekta hizi yanahitaji viongozi wenye dira, ufanisi na uwajibikaji,” amesema Dk. Buriani.
Ameeleza kuwa kupitia jukwaa la Business to Business (B2B), wakulima, wafugaji na wavuvi walipata mafunzo ya kina kuhusu mnyororo wa thamani, ufungashaji bora, masoko, fursa za kifedha na matumizi ya teknolojia, huku watafiti, wazalishaji na wanunuzi wakileta mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya maji yenye upatikanaji wa saa 24 umeifanya Morogoro kuwa na mazingira bora ya kufanikisha maonesho endelevu.
“Kuanzia sasa, eneo hili la Nanenane litakuwa soko la mbogamboga kila Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,” amesema Malima.
Aidha, ameeleza kuwa kuna mpango kabambe wa kuligeuza eneo hilo kuwa kituo cha burudani na maonesho ya wanyama hai, hatua itakayoongeza shughuli za kiuchumi na kuvutia wawekezaji na watalii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED