Bashe: Wagombea wasihadae wananchi kuhusu mifumo ununuzi wa mazao

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 05:03 PM Aug 08 2025
 Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Mtandao
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Serikali imewaonya wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao dhidi ya kuwarubuni wananchi kwa ahadi za kuondoa mifumo ya ununuzi wa mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani na minada ya kidijitali, kwa madai kuwa mifumo hiyo ni mzigo kwa wakulima.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ambaye pia amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kukemea vikali tabia hiyo, akisema kuwa mifumo hiyo imebuniwa mahsusi kusaidia wakulima na kukuza uchumi wa taifa.

“Naomba wananchi wasikubali kurubunika. Rais tunaomba utusaidie kukemea hili. Hii mifumo ina manufaa kwa serikali na wananchi kwa ujumla,” amesema Bashe.

Bashe amefafanua kuwa mifumo ya stakabadhi ghalani na minada ya kidijitali inaisaidia serikali katika ukusanyaji sahihi wa mapato, huku ikiisaidia TRA kuwa na takwimu sahihi za ununuzi wa mazao, na kwa upande wa wakulima, inahakikisha vipimo sahihi na bei stahiki za mazao yao.

Amesema baadhi ya wagombea wamekuwa wakipinga mifumo hiyo ili kukwepa kodi, jambo ambalo linaathiri maendeleo ya sekta ya kilimo na kunyima wakulima haki zao.

Serikali kuendelea kununua mahindi, soko la mbaazi latafutwa

Akizungumzia suala la uzalishaji wa mahindi, Bashe amesema kuwa serikali imepanga kuzalisha tani milioni 10 mwaka huu, na akawahakikishia wakulima kuwa hakuna zao litakalooza au kukosa soko.

“Niwatoe hofu wakulima, serikali itaendelea kununua mazao yao. Hakuna mazao yatakayo haribika,” amesisitiza.

Kuhusu kushuka kwa bei ya mbaazi, Waziri Bashe amesema kuwa serikali tayari imeanza mazungumzo na Serikali ya India kwa lengo la kutafuta soko la kudumu la zao hilo, ambalo limekuwa likiwaingizia kipato wakulima wengi nchini.

Amefafanua kuwa bei ya mbaazi imepanda kutoka Sh 200 hadi Sh 1,200 kwa kilo, na akatoa rai kwa wakulima kuwa watulivu na kuendelea kulima kwa bidii kwani serikali iko pamoja nao.

“Tunataka kilimo chenye tija, chenye masoko ya uhakika, na serikali imejipanga kuhakikisha hilo linafanikiwa,” amesema Bashe.