Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amezitaka Halmashari nchini kuweka mikakati ya kupambana na ndege waharibifu wa mpunga (kwelea kwelea) shambani na kufanya wakulima kuona tija ya kilimo.
Malima amesema hayo wakati alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero akiwa kwenye ziara katika mabanda ya maonesho ya kilimo 88 kanda ya mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro.
Malima aliipongea Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa jitihada za kuteketeza mazalia ya ndege hao na kufanya hali ya utulivu kwenye mashamba ya mpunga.
Afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Emmanuel Salim anasema ndege hao waharibifu huwa na uwezo wa kula kilogramu 5.0 kwa saa mara wanapoingia shambani sababu wamekuwa wakila mazao hayo yakiwa katika hatua ya maziwaziwa huku wakiwa kwenye makundi makubwa ya ndege hadi kufikia zaidi ya Milioni moja kwa kundi moja.
Anasema wilaya hiyo imejipanga kuchukua hatua stahiki pindi watakapoona ndege hao wanaanza tu kutokana na kutenga kitengo maalum ambacho wanashirikiana na Serikali kuu kuhakikisha mazao ya mkulima yanakuwa salama.
Mmoja wa wakulima kutoka Dakawa wilayani humo Hamisi Mpanga alipotembelea banda hilo aliishukuru serikali kwa jitihada zake za kutoa ndege yenye dawa kwa ajili ya kuua ndege hao waharibifu wakati wa msimu wa kilimo cha mwaka 2024/25 mapema na kufanya kufanikiwa katika mavuno ya msimu huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED