NIDA kuzindua mfumo mpya wa kufuatilia maombi ya vitambulisho

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 01:12 PM Aug 08 2025
NIDA kuzindua mfumo mpya  wa kufuatilia maombi ya  vitambulisho
Picha: Mpigapicha Wetu
NIDA kuzindua mfumo mpya wa kufuatilia maombi ya vitambulisho

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kuzindua mfumo mpya wa kidijitali utakaowawezesha wananchi kufuatilia maendeleo ya maombi ya vitambulisho vyao kwa kutumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kupitia simu za mkononi.

Akizungumza na vyombo vya habari katika banda la NIDA kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NIDA, Geofrey Tengeneza, amesema mfumo huo utatumia CODE maalum itakayomuwezesha mwananchi kupata taarifa zake moja kwa moja bila gharama yoyote.

“Mfumo huu utarahisisha huduma na kumuwezesha mwananchi kujua hatua iliyofikiwa ya maombi yake ya kitambulisho bila kufika ofisi za NIDA,” amesema Tengeneza.

Aidha, Tengeneza alieleza kuwa kupitia maonesho hayo, NIDA inaendelea kutoa elimu kuhusu mfumo huo mpya, pamoja na huduma nyingine kwa wakulima, wafugaji na wananchi wanaohudhuria. Elimu hiyo inahusiana na taratibu za usajili, viambatisho vinavyohitajika wakati wa usajili, na matumizi ya mfumo wa usajili wa mtandaoni (e-registration).

Kwa mujibu wa Tengeneza, hadi kufikia Agosti 6, zaidi ya wananchi 700 walikuwa tayari wamehudumiwa katika banda la NIDA tangu kuanza kwa maonesho hayo, jambo linaloonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi kutaka kupata huduma na elimu ya utambulisho wa taifa.