Macho, masikio Dodoma Dk. Samia akichukua fomu kesho

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:42 PM Aug 08 2025
 Dk. Rais Samia Suluhu Hassan
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Rais Samia Suluhu Hassan

Mgombea wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi wa urais katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kesho Agosti 9, 2025 jijini Dodoma.

Hatua hiyo inamfanya kuwa mgombea wa kwanza wa wadhifa huo kuchukua fomu, huku wagombea wa nafasi hiyo kutoka vyama vingine wakitarajiwa kufanya hivyo katika siku za karibuni kulingana na ratiba ya INEC.

Sambamba na hilo, hatua hiyo inaandika historia ndani ya CCM, kwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya urais INEC, tangu kuasisiwa kwa chama hicho 1977, ukiacha wale waliowahi kutiania na kuishia kwenye michakato ya ndani ya chama hicho.

Kuchukua fomu kwa mkuu huyo wa nchi, kutamfungulia pazia la kuanza safari za kusaka kura katika kampeni zitakazoanza Agosti 28, hadi Oktoba 28 kisha siku inayofuata Watanzania watapiga kura za kuwachagua wabunge, madiwani na Urais.

Macho na masikio yote kesho saa 5:00 asubuhi yatakuwa Ofisi za INEC zilizopo Ndenjengwa jijini Dodoma wakati Dk Samia atapoweka historia ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwatumikia Watanzania kwa miaka mitano ijayo.

Dk. Samia anachukua fomu hiyo, akiwa amebeba matumaini makubwa ya kuwahudumia na kutatua kero zinazowakabili Watanzania kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/30 iliyosheheni vipaumbele tisa ikiwemo kuboresha maisha ya watu.

Hata hivyo, Rais Dk. Samia anachukua fomu hiyo akiwa na rekodi ya kuhudumu kwa miaka minne katika wadhifa wa urais wa Tanzania, tangu Machi 19, 2021.

Hatua ya kuingia kwake madarakani, ilitokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa Rais wa wakati huo, hayati Dk. John Magufuli, Machi 17, 2021.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais Dk. Samia ambaye kwa wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, akaapishwa kuwa Rais na kuhudumu kwa kipindi cha miaka minne.

Kuingia kwake madarakani, kuliandika historia ya Tanzania kuwa na Rais wa kwanza mwanamke na utendaji wake mzuri, umevunja mitazamo kuwa, uongozi si jinsia, bali ufanisi, weledi na uchapakazi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema Dk. Samia ataambatana na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi katika safari hiyo ya kuchukua fomu.

Amesema nje ya jengo la CCM Makao Makuu, shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo ujenzi wa jukwaa maalum atakalolitumia Rais Dk. Samia kuzungumza na wanachama, baada ya kuchukua fomu.