Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura, amewaonya Watanzania wasikubali kudanganyika na kushawishiwa na watu kutoka ndani na nje ya nchi kuvuruga amani ya taifa.
Pia, amewasihi Watanzania asitokee mtu yeyote akawadanganya na wakakubali kudanganyika.
Alitoa angalizo hilo jana wakati akizungumza katika wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro akishiriki ufunguzi wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Daraja B, kilichopo Mji Mdogo wa Sanya Juu.
“Thamani ya usalama wetu ni kubwa kuliko kipato chetu. Naomba nitumie jukwaa hili kuwakumbusha Watanzania. Kuvuruga amani ya nchi ni suala la dakika moja.
…Kuirudisha amani ya nchi gharama yake ni kubwa sana. Tunazifahamu nchi ambazo zimepoteza amani, utulivu na usalama wa nchi zao. Kuna baadhi ya majirani zetu, gharama ya kurudisha amani imeshindikana.” alisema.
Ufunguzi wa kituo hicho, ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuimarisha miundombinu ya Jeshi la Polisi nchini, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za usalama na ulinzi kwa wananchi.
Akizungumza kabla ya kufungua kituo hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alimtaka Mkuu wa Jeshi hilo la Polisi, kuboresha doria za mtandaoni kama inavyofanyika mitaani, ili kudhibiti uhalifu wa kifedha na wanaohamia kwenye mtandao kuvuruga amani.
Waziri Bashungwa alisema: “Nikuombe IGP, sasa hivi wahalifu wengine wamehamia mtandaoni. Kama ambavyo mnafanya ukaguzi wa mitaa, tuimarishe online patrol; ili kuweza kudhibiti uhalifu wa wizi wa kifedha lakini pia na wahalifu wanahamia kwenye mitandao kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu.
…Kwa hiyo hili IGP, kama ambavyo mnafanya kazi nzuri ya kuhakikisha mitaa na vijiji vinakuwa salama kwa kufanya ukaguzi zinazoonekana, lakini wahalifu ambao wamehamia mtandaoni naomba mwendelee kushughulika nao bila kuwaonea muhali.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED