MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi wamefika katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo.
Uchukuaji fomu huo umefanyika leo mkoani Dodoma, ambako pia wananchi mbalimbali makada wa chama hicho wamejitokeza kwa wingi katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM, wakimsubiri Mgombea Urais Samia, pamoja na mgombea mwenza Balozi Dk. Nchimbi, kwa ajili ya kuzungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Wananchi hao wameonekana wamejaa barabarani wakiwa wameshika mabango yenye jumbe mbalimbali ikiwemo 'Oktoba tunakiti' huku wakisubiri kwa hamu msafara wa wagombea hao kutoka Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa.
Tukio hilo limepambwa na burudani kutoka kwa wasanii maarufu nchini, Mboso na Dulla Makabila, waliotumbuiza wakati wananchi na wanachama wa CCM wakiendelea kujumuika na kusubiri kuwasili kwa wagombea hao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED