MAMLAKA ya dawa na vifaa tiba ( TMDA ) imetumia maonyesho ya saba ya Kilimo na Ufugaji Kanda ya Ziwa Magharibi kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitenganishi.
Akizungumza jana Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki (Mwanza), Aggrey Muhabuki, alisema mamlaka hiyo ilishiriki kwenye maonyesho hayo kwa kushirikisha wataalamu mbalimbali waliotoa ufafanuzi wa masuala ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba.
“Tumeweza kuwaeleza wadau namna sahihi ya kutumia dawa na vifaa tiba, sambamba na kutoa tahadhari kuhusu athari za matumizi mabaya, hasa kwa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi,” alisema.
Alifafanua kuwa maonyesho hayo yamewapa fursa ya kukutana ana kwa ana na wakulima, wafugaji na wavuvi, na kuwapa elimu kuhusu jinsi ya kutumia dawa ipasavyo ili kulinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uwezekano wa kuibuka kwa vimelea vinavyozalisha sumu endapo dawa za mifugo zitatumika vibaya TMDA pia ilitembelea mabanda ya washiriki kuchukua taarifa za wadau hao, ili kupanga ratiba ya kuwatembelea na kuwafundisha zaidi.
“Tutapanga ndani ya mpango kazi wetu kuwafikia mara kwa mara kwa elimu ya matumizi sahihi ya dawa tumebaini kuwa dawa zimekuwa zikitumika kunenepesha mifugo, jambo ambalo lina athari kubwa kwa afya za walaji,” aliongeza.
Aidha, TMDA ilikumbusha kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mifugo yanaweza kuathiri mazao yake kama nyama, maziwa na mayai, hasa pale ambapo hayaheshimiwi masharti ya kusubiri muda maalumu kabla ya kuyatumia baada ya kutoa tiba kwa mnyama.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja huyo, elimu endelevu kwa wadau wote wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ni muhimu ili kuhakikisha matumizi ya dawa yanafuata miongozo ya kitaalamu na kulinda afya ya jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED