Mwalimu mkuu auwawa kikatili na wasiojulikana nyumbani kwake

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:48 PM Aug 09 2025
news
Picha Shabani Njia
Ndugu, jamaa na marafiki wakiomboleza kifo cha mwalimu huyo.

MWALIMU Mkuu wa shule ya msingi Busalala iliyopo kata ya Mwendakulima Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Salumu (41), anadaiwa kuwawa na watu wasiojukana kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni mwake, huku mume wake akishikiliwa na polisi kwa kuhusishwa na tukio hilo.

Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga SACP. Janeth Magomi amethibitisha leo tukio hilo linalodaiwa kutokea jana August 8, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku huku chanzo kikielezwa ni ugomvi wa familia baina ya marehemu na mume wake.

Amesema, mwili wa mwalimu huyo ulikutwa nyumbani kwake akiwa ameuwawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni kulia na watu wasiojulikana na umehifadhiwa katika hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku upelelezi ukiendelea.

“Tukio hili ni lakusikitisha sana na nilakikatili na halifai kuendelea kuvumilika kwenye jamii, tutaendelea kuwatafuta wale wote wanaodaiwa kuhusika na tukio hili ili sheria iweze kuchukua mkondo wake hivyo niwaombe wanandoa au wanafamilia kuacha kujichukulia sheria mkononi,” ameongeza Magomi.

Balozi wa mtaa wa Budushi Kata ya Mwendakulima Rashidi Charles amesema, taarifa za tukio hilo alizipata majira ya saa 8:00 usiku na alipofika kwenye eneo la tukio alikuta mwili wa marehemu ukiwa chini ya sakafu kando ya kitanda ukiwa umechomwa na kitu chenye nchi kali shingoni na damu zikionekana kutapakaa sakafuni.

Aidha, amesema, alitoa taarifa katika vyombo vya dola na vilifika na kumchukua mwili wa marehemu na kuondoka nao, na kwamba tukio hilo ni la tatu kutokea kwakuwa la kwanza na yote yanafanana ya kuuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, akitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuingilia kati na kutatua tatizo hilo lisiendelee kujitokeza tena.

Naye, Mwalimu wa shule ya msingi Mwendakulima Magreth Mwandu amesema, amefanyakazi na marehemu katika shule hiyo kabla ya kuwa Mwalimu Mkuu shule ya msingi Busalala na hakuwa na tatizo na watu kwani walikuwa wakishirikiana vyema kwenye jamii na katika michezo yao ya hisa.