Samia: CCM iko tayari kwa kampeni

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 05:00 PM Aug 09 2025
news
Picha Renatha Msungu
Rais Samia Suluhu Hassan na Mgombea mwezi Bolozi Dk Emmanuel John Nchimbi wakiwaonyesha wanachama wa chama cha mapinduzi mkoba uliobeba fomu ya kugombea Urais baada ya kukabidhiwa na Tume huru ya Uchaguzi leo

MGOMBEA nafasi ya Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema, mbio za kuelekea Oktoba sasa zimeanza na Agosti 28 wanafungua rasmi kampeni na kuhitimishwa Oktoba 28 kusubiri wananchi wanasemaje.

Samia amesema hayo leo katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM saa chache baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais yeye na mgombea mwenza Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

Amesema wako tayari kuicheza ngoma kwa namna yeyote itakavyopigwa na kusema wako tayari kwenda kufanya kazi walioagizwa na Chama.

Pia Samia amesema, katika Dira ya 2050 wanakwenda kuitekeleza kwa kufanya mambo makubwa ili kuhakikisha Tanzania inasonga mbele na kupiga hatua katika maendeleo ikiwemo kufanya taifa linalojitegemea kwenye uchumi.

Amesema kwa upande wao chama Cha Mapinduzi wanakwenda kutekeleza hayo kwa asilimia kubwa kwa sababu serikali kupitia CCM wanauwezo mkubwa na uzoefu.

Amesema fomu hiyo ya uchaguzi itapelekwa mikoa yote kwa ajili ya kuombea udhamini na kuwaomba kufanya vizuri kwenye hilo.

Naye, mgombea Mwenza wa nafasi ya Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Mchimbi amesema anamshukuru Rais Samia kwa kumteua kuwa mgombea mwenza huku akimuhakikishia kukitafutia chama ushindi wa kishindo na amejiandaa kuwa msaidizi wake na sio kuwa mshindani wake.