BAADHI ya wakazi na watumiaji wa barabara kuu ya Arusha–Moshi kuelekea Dar es Salaam, hususan katika kata za Kileo na Hedaru mkoani Kilimanjaro, wamesema juhudi za serikali kukarabati miundombinu ya barabara zitasaidia kuondoa tatizo la mafuriko na maji kujaa barabarani nyakati za mvua.
Wakizungumza Nipashe kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya siku moja ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakazi hao walisema tatizo la maji na magogo kufunika barabara limekuwa likisababisha usumbufu mkubwa, ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa safari, uharibifu wa mali na wakati mwingine vifo.
Mmoja wa wakazi, Hasani Msuya, alisema nyakati za mvua huwa ni changamoto kufika maeneo ya huduma muhimu kwa sababu ya maji na magogo yanayoziba barabara, jambo linalosababisha shughuli za kiuchumi kudorora.
“Hapa Kileo maji yalikuwa yanaweza kukaa saa nne au tano. Unabeba abiria wanaokwenda kwenye biashara au matibabu, lakini wanachelewa barabarani. Hii inapelekea kudidimia kwa uchumi wa taifa,” alisema Msuya.
Naye mkulima wa Kileo, Yusufu Seleman, alisema tatizo hilo limekuwa ikisababisha hasara kubwa ya mazao mashambani, huku mafuriko yakiwa tishio la maisha na makazi.
“Mwaka 2016 tuliletewa chakula kwa msaada kutokana na mafuriko. Kukamilika kwa kalvati hivi kutatusaidia sana msimu wa mvua, ila tunaomba pia serikali ichimbe njia kuelekea mto uliopo karibu ili maji yapite moja kwa moja na yasizagaa kwenye mashamba,” alisema Seleman.
Aliongeza kuwa wakati wa mvua kali, baadhi ya wakazi hulazimika kuhama makazi kwa kuhofia usalama wao, huku wanafunzi wakishindwa kwenda shule na familia kushindwa kupata mahitaji muhimu.
“Wapo waliopoteza maisha, mfano mvua za 2023/2024 ilidaiwa watu watatu walifariki na wawili walipotea hadi leo hawajulikani walipo,” alisema Seleman.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alikagua ujenzi wa boksi kalvati saba katika eneo la Kileo, mradi wenye thamani ya milioni 6.8 unaotekelezwa na mkandarasi KINGS. Ujenzi huo umefikia asilimia 31.
Aidha, katika Wilaya ya Same, kulikaguliwa pia mradi wa ujenzi wa daraja wenye thamani ya bilioni 1.5, unaotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji katika maeneo yaliyoathirika na mvua kubwa.
Kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, TANROADS imepata ufadhili wa bilioni 16.2 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja, njia za maingiliano na usimamizi wa miradi ya dharura.
“Miradi hii inalenga kurejesha hali ya barabara zilizoharibiwa na mvua za Elnino, na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao bila vizuizi vya miundombinu,” alisema Kyando.
Mkuu wa Mkoa, Babu, aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili miradi ikamilike kabla ya mvua za vuli kuanza, na kuwataka wananchi kushirikiana katika kutunza miundombinu hiyo.
“Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa iliyoathirika zaidi na mvua za Elnino za 2023 na 2024, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunajenga miradi ya kudumu na inayostahimili changamoto za hali ya hewa,” alisema Babu.
Kwa sasa, miradi hiyo ya dharura inatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la usafiri na usafirishaji katika maeneo yaliyokuwa yakikumbwa na mafuriko, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi katika mkoa wa Kilimanjaro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED