Ratiba uchaguzi Zanzibar mbioni kuwekwa wazi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 04:21 PM Aug 09 2025
news
Picha Mtandao
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Thabit Idarous Faina.

TUME ya Uchaguzi Zanzibar imesema inatarajia kutangaza ratiba ya uchaguzi baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi ambalo linatarajiwa kuvunjwa Agost 13, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kando ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya wilaya yaliyolenga kuwajengea uwezo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Thabit Idarous Faina, amesema kuwa wanatarajia kutoa taarifa rasmin Agost 18, mwaka huu ili kutoa ratibaba nzima ya uchaguzi.

Miongoni mwa ratiba ya maandalizi ya uchaguzi mkuu itakayotolewa na tume hiyo ni pamoja na siku ya kupiga kura pamoja na zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa wagombea.

Faina pia amesema baada ya siku tano za kuvunjwa kwa Baraza la wawakilishi ambalo litafikia ukomo wake Agost 13 mwaka huu watatangaza ratiba hiyo ambako pia Agost 24 mwaka huu itakuwa ni siku ya kusaini maadili ya kampeni za uchaguzi kwa vyama vya siasa.

Akizungumzia kuhusu mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya wilaya,Faina amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha maofisa uchaguzi wa wilaya kufanya kazi zao kwa uadilifu na umakini mkubwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Amesema maofisa hao ndio wenye dhamana kubwa ya shughuli zote za kiuchaguzi na kiunganishi baina ya tume, maofisa wasaidizi wa majimbo na ngazi ya vituo.