MASHIRIKA ya Kiraia kutoka Afrika yameandamana mbele ya jengo la Umoja wa Mataifa kudai mkataba wa Kimataifa wa Kisheria wa Plastiki wenye nguvu ya kuwalinda dhidi ya taka za plastiki.
Maandamano hayo yalifanyika juzi katika eneo la Place des Nations jijini Geneva, Uswisi, yanapofanyika majadiliano ya kiserikali ya kuandaa mkataba huo yaliyoanza Agosti 5, mwaka huu, yanaendelea kwa siku 10.
Waandamanaji hao walivaa nguo za njano, nyekundu na machungwa kusisistiza dharura dhidi ya janga la plastiki ambalo linaathiri afya za wanadamu na mazingira.
Waandamanaji hao pia walishikilia mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo kushughulikia kwa haraka uzalishaji wa plastiki usiodhibitiwa.
Mmoja wa waandamanaji Mkuu wa Mradi wa Plastiki wa Pan-Afrika kutoka shirika la Greenpeace Afrika, Hellen Dena, alisema licha ya kuwa Afrika inazalisha kiasi kidogo cha taka za plastiki, lakini inabeba mzigo mkubwa wa taka kutoka mataifa tajiri zinazoathiri afya na mazingira ya bara hilo.
"Jamii zetu zinaelea kwenye bahari ya taka za plastiki huku tukichangia sehemu ndogo tu ya uzalishaji wake duniani. Tunahitaji mkataba utakaoanza kudhibiti tatizo hili kutoka chanzo chake kwa kupunguza uzalishaji badala ya kuhamishia mzigo kwa wale wasiohusika," alisisitiza.
Dana alilisitiza kuwa mkataba huo unapaswa kuwatambua waokota taka ambao wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 20 duniani, wengi kutoka Afrika.
Alisisitiza nchi wanachama kutoka Afrika kusimamia msimamo wa pamoja wa kupunguza uzalishaji wa plastiki kwa kiwango kikubwa katika mzunguko mzima wa maisha ya plastiki kutoka utengenezaji hadi utupaji.
"Ni wakati wa kumaliza enzi ya plastiki. Mkataba huu ni fursa ya kihistoria ya kulinda afya zetu, jamii zetu na sayari kwa ujumla," alisema Dena.
Mtaalamu urejeshaji taka wa kutoka taasisi ya Greenpeace Switzerland, Joëlle Hérin, alisema maandamano hayo yanalenga pia kuishinikiza nchi ya Uswizi kuwa na msimamo thabiti kuhakikisha kuwa mkataba huo unakamilika ndani ya siku kumi na unakuwa matokeo tarajiwa.
"Kwa kuwa Uswisi ni mwenyeji wa mazungumzo haya, tunatarajia ichukue msimamo thabiti. Kwa kasi ya sasa ya uzalishaji wa plastiki, inakadiriwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050. Mkataba wowote usio na lengo la kimataifa la kupunguza uzalishaji huo ni sawa na kushindwa kabla hata haujaanza kutekelezwa.”
Mkurugenzi wa Shirika la Utu na Mazingira (HUDEFO) Sarah Pima, alisema pia kuna haja ya mkatanba unaoandaliwa uoanishwe na ile ya Basel na Bamako inayolenga kudhibiti utupaji haramu wa taka hatarishi barani Afrika.
Alipongeza nchi za Rwanda na Ghana ambazo katika majadiliano ya kuandaa mkataba huo yaliyotangulia zilionesha uongozi kwa kupendekeza mipaka ya uzalishaji wa plastiki na kufutwa kwa plastiki hatarishi.
Alisema Tangu China ilipopiga marufuku uagizaji wa taka za plastiki mwaka 2018, Afrika imekuwa dampo la taka hizo, hali inayotengeneza maeneo yenye sumu yanayohatarisha afya, ardhi, maji, na hewa ya wakazi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Inger Andersen, alisema kuwa mifumo ya kisheria ya kimataifa tayari ipo kukabiliana na tatizo la utupaji wa taka za plastiki barani Afrika.
Aliitaja mikataba hiyo kuwa ni wa Basel ambao umeainisha aina za plastiki ambazo ni hatarishi na zimezuiliwa kusafirishwa kuvuka mipaka na Mkataba wa Rotterdam, unaotaka kuwepo kwa ridhaa ya awali ya nchi husika kabla ya kusafirisha taka hatarishi.
“Lazima nchi husika ikubali kupokea taka hizo kabla hazijasafirishwa. Hivyo basi, fursa ya kutupa taka kiholela bila idhini imepungua kwa kiasi kikubwa,” aliongeza.
Andersen pia alisisitiza mkataba unaoandaliwa ukiwa madhubuti utasaidia kuvutia uwekezaji na kuharakisha mabadiliko kuelekea uchumi mzunguko.
“Mkataba huu ni wa muhimu sana kwa sababu pale ambapo sheria za kimataifa juu ya usimamizi wa plastiki zinapowekwa, wawekezaji hupata uhakika. Wanajua kuna soko la kile kinachokusanywa, na kwa sababu hiyo kutakuwepo na uwekezaji. Kitu kinachoonekana kuwa taka leo, kinaweza kuwa chenye thamani kesho,” alisema.
Hata hivyo, Andersen alisema kuwa sehemu kubwa ya uchafuzi wa plastiki unaoonekana sasa unatokana na uzalishaji wa ndani ya nchi hizo.
Takwimu kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) zinaonesha kuwa plastiki ina zaidi ya kemikali 16,000, ambapo takribani 4,200 kati ya hizo ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED