Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wakulima kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki na kujifunza kupitia maonesho ya wakulima maarufu kama Nanenane, ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Chalamila ametoa wito huo leo wakati akitembelea maonesho ya wakulima ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Kata ya Tungi, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema Serikali kwa sasa imewekeza mabilioni ya shilingi katika sekta ya kilimo, kwa lengo la kuwahudumia Watanzania kupitia matumizi ya mbegu bora, pembejeo sahihi, na teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao kwa manufaa ya ndani na kuuza nje ya nchi.
“Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao, ili waingie kwenye soko la ushindani kimataifa. Tunahitaji kuona bidhaa zetu za kilimo zikisafirishwa nje, jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa Taifa,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, Mratibu wa Masuala ya Jamii kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk. Faraja Bilahi, amesema taasisi hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
Ameeleza kuwa IHI imejikita kusaidia jamii ya wakulima kwa kuhakikisha wanakuwa na afya bora, hasa kwa kupambana na ugonjwa wa malaria kwa kutumia tafiti za kitaalamu ili kumaliza kabisa mbu waenezao ugonjwa huo.
Naye Mtafiti kutoka Ifakara Health Institute, Pinda Polias, ameonya juu ya matumizi holela ya viuatilifu mashambani vinavyoweza kuleta usugu kwa mbu dhidi ya dawa zinazotumika katika vyandarua.
Amesisitiza umuhimu wa wakulima kutumia dawa za malaria kwa usahihi na kuhakikisha mgonjwa anapona, kwani maeneo ya kilimo ndio mazalia makuu ya mbu.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ilonga (MATI-Ilonga), Felix Mrisho, amewataka wadau wa kilimo kutembelea banda la chuo hicho kujifunza teknolojia za kisasa za uzalishaji na usindikaji wa mazao.
Amesema wakulima hawapaswi kuuza mazao ghafi moja kwa moja kutoka shambani, bali wanatakiwa kuyaongezea thamani kwa kuyasindika ili kujipatia kipato kikubwa zaidi.
“Ukisindika mazao yako unapata faida kubwa zaidi kuliko kuuza mazao ghafi. Tunawakaribisha wakulima wote katika banda letu wajifunze mbinu bora za kuongeza thamani na kukuza uchumi wao,” alieleza Mrisho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED