THRDC yatoa mafunzo kwa watetezi wa haki za watoto

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 09:16 AM Aug 07 2025
Wakili Paul Kisabo akizungumza na watetezi wa haki za watoto mkoani Dodoma.
Picha:Mpigapicha Wetu
Wakili Paul Kisabo akizungumza na watetezi wa haki za watoto mkoani Dodoma.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeendesha mafunzo ya siku mbili kwa mashirika na taasisi zaidi ya 40 zinazotetea haki za watoto nchini, kwa lengo la kuwaelimisha na kuwakumbusha wajibu wao katika uandaaji wa ripoti kivuli zinazohusu hali ya haki za watoto.

Mafunzo hayo yamefanyika jijini Dodoma na yamelenga kuimarisha uelewa kuhusu kanuni, sheria na miongozo ya kimataifa na kikanda inayosimamia haki za watoto, pamoja na kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa huko nyuma kwenye taasisi za kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Utetezi kutoka THRDC, Wakili Paul Kisabo, amesema kuwa mafunzo hayo yamewalenga zaidi wanachama wapya wa mtandao wanaojihusisha na utetezi wa haki za watoto ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji na kuwaweka kwenye mstari mmoja wa uelewa.

“Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayohusiana na haki za watoto, ambayo inaitaka serikali kuwasilisha taarifa ya hali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kila baada ya miaka minne au mitano. Hivyo, mashirika haya yana jukumu la kuandaa ripoti kivuli zitakazosaidia kufuatilia utekelezaji wa haki hizo,” amesema Wakili Kisabo.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki wamefundishwa namna ya kufuatilia utekelezaji wa sheria, kuandaa ripoti kwa kutumia mifumo husika, na pia kufanya mapitio ya mapendekezo ya awali ili kubaini maendeleo yaliyopatikana au changamoto zinazobaki.

Kwa upande wake, Mratibu wa THRDC Kanda ya Kati, Bi. Sharon Kabunga, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa mashirika na taasisi zinazoshiriki katika utetezi wa haki za watoto, huku yakisaidia kupanua uwezo wao katika kushiriki miradi ya kitaifa na kimataifa.

“Wadau wengi wameonyesha mafanikio makubwa baada ya kushiriki mafunzo haya, kwani sasa wanaweza kutetea haki za watoto kwa weledi zaidi, na hata kupata fursa za miradi mbalimbali inayolenga kuboresha maisha ya watoto hapa nchini,” amesema Kabunga.

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za THRDC kuhakikisha kuwa sauti ya mashirika ya kiraia inasikika katika muktadha wa kimataifa na kwamba haki za watoto zinalindwa ipasavyo kwa kushirikiana na taasisi za serikali na kimataifa.