Tume ya Uchaguzi: Wasimamizi tendeni haki bila upendeleo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:06 PM Aug 07 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa haki, bila upendeleo kwa vyama au wagombea, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wenye uwazi.

Jaji Mwambegele ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, ngazi ya kata, kutoka Halmashauri za Wilaya ya Kyela na Rungwe, mkoani Mbeya.

“Mnapaswa kutenda haki kwa vyama vyote na wagombea wote. Hili litasaidia kuondoa malalamiko, kujenga imani kwa wadau na kuimarisha demokrasia nchini,” amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.

Aidha,Jaji Mwambegele aliwakumbusha wasimamizi hao umuhimu wa kuviishi viapo vyao kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Tume, ili kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi unafanyika kwa weledi na uadilifu.