WAKULIMA na wafugaji, wanaosafirisha mifugo na mazao nje ya nchi, wametakiwa kuchangamkia fursa maonesho ya Nanenane, kusajili na makundi yao, ili watekeleze majukumu vyema pasipo kusumbuliwa.
Ofisa Leseni Mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA), Rehema Kionomela, amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.
Rehema amesema BRELA wamesogeza huduma hiyo kwa wakulima, ikiwa na pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaoshindwa kufika katika ofisi hizo.
Amezitaja huduma zinazotolewa viwanjani hapo ni pamoja na usajili wa kampuni, jina la biashara, alama za biashara na huduma, usajili wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo pamoja na utoaji leseni kundi ‘A’ zenye sura ya kitaifa na kimataifa
Ametoa wito kwa wananchi kuutumia mfumo wa ORS na TNBP, ili kujisajili kwa kuwa mfumo ni rahisi na unaelekeza hatua za kufuata.
Farid Hoza, Ofisa Kumbukumbu kutoka taasisi hiyo, amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa na tofauti, kwa kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wakulima kufika katika banda hilo.
“Licha ya kuwa changamoto ya wananchi kutokua na uelewa wa kutosha wa jinsi ya kuhuisha taarifa za majina na kampuni zao, kufika na viambata pungufu na kutokufahamu matumizi ya mfumo,” amesema.
Mmoja kati ya wananchi waliotembelea banda hilo, Hamadi Kodelo, mkazi wa Dodoma, anayefanya shughuli zake mkoani Manyara, aliishukuru BRELA kwa kumhudumia kwa wakati na kuondoka na leseni yake papo hapo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED