Kilosa wamshukuru Rais Samia kuwafikishia nishati safi ya kupikia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:03 PM Aug 06 2025
Kilosa wamshukuru Rais Samia kuwafikishia nishati safi  ya kupikia
Picha; Mpigapicha Wetu
Kilosa wamshukuru Rais Samia kuwafikishia nishati safi ya kupikia

Wananchi Wilayani Kilosa mkoani Morogoro wameshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia mradi unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa kusambaza majiko yaliyoboreshwa maarufu kama majiko banifu kwa bei ya ruzuku ya shilingi 14,700 kwa kila jiko.

Wametoa shukrani hizo Agosti 6, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi shilingi bilioni 9.4 wa kusambaza majiko banifu ambayo yatasambazwa kote nchini kwa bei ya ruzuku uliyofanyikia eneo la Stendi wilayani humo ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaka Hamdu akiwa mgeni rasmi.


“Rais Samia ni mkombozi wetu, sisi wajasiriamali ametusaidia sana, kwanza alituletea majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku na sasa tumepokea majiko haya banifu ambayo nayo yanakwenda kuwa msaada mkubwa kwa shughuli zetu za kila siku,” alisema Daines Samwel ambaye ni mjasiriamali eneo la Stendi ya Kilosa.


Naye Aisha Swai, mkazi wa Uhindini wilayani humo alisema majiko haya yanakwenda kupunguza gharama za maisha kwani hapo awali alikuwa akitumia zaidi ya shilingi 20,000 kununua mkaa kwaajili ya shughuli zake siku za mama lishe na kwamba kutokana na sifa ya majiko hayo ya kutumia mkaa mchache itamsaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli zake.

Akizindua mradi, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu alisema Wilaya ya Kilosa ni mnufaika mkubwa wa miradi inayosimamiwa na REA na aliipongeza kwa kuendelea kutekeleza na kusimamia maono na maelekezo ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ya usambazaji wa umeme na usambazaji wa nishati safi ya kupikia.


“Kwa hapa Kilosa, tunashukuru sana, vijiji vyote vimefikishiwa umeme na kazi inaendelea ya kufikisha umeme kwenye vitongoji; leo hii tupo hapa kuzindua mradi mkubwa wa zaidi ya shilingi bilioni tisa wa majiko banifu yanayotolewa kwa bei ya ruzuku,” alisema Hamdu.


Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia mradi huo ambao alisema ni suluhu ya uharibifu wa misitu inayoizunguka wilaya hiyo lakini pia ni mkombozi wa afya za wananchi hao ambao wamekuwa kwa kiwango kikubwa wakikata miti kwa ajili ya kuni za kupikia.


“Ndani ya wilaya ya Kilosa unaweza kusema kwa 100% wananchi wamekuwa wakitumia nishati isiyosalama, nishati ambayo siyo sahihi; tuliona njia nyepesi ni kutumia kuni lakini kumbe mambo yamebadilika misitu yetu inapaswa kubaki salama na afya zetu pia kutoathirika tena na moshi wa kuni,” alisisitiza Hamdu.


Akizungumzia mradi kwa ujumla wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema kuwa REA imejipanga kikamilifu kuhakikisha lengo lililomo katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia linafikiwa.


“Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imetambua changamoto wanayopata wananchi wake na ndio sababu imeweka ruzuku kubwa ili kuwafikia wananchi wengi Zaidi. Miti inakatwa kwa wingi, akina mama na watoto wanapata madhara kiafya na ili kuondokana na madhara haya tumejuka na majiko banifu nchi nzima na kwa kuanzia kwa hapa Morogoro kila wilaya itafikishiwa majiko 1,195,” alifafanua Mha. Advera.


Alibainisha kuwa kampuni saba zimeshinda zabuni za kusambaza majiko banifu katika mikoa mbalimbali kote nchini na kwamba kila mwananchi mwenye kuhitaji jiko banifu kupitia mradi huo anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa ili kuiwezesha Serikali kutunza kumbukumbu na kupata takwimu halisi ya utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia.

Mhadisi Advera alibainisha kuwa mradi huo wa majiko banifu unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali na Jumla ya majiko 200,000 yatasambazwa nchi nzima.

Alisema REA itaendelea kutekeleza miradi ya Nishati Safi ya kupikia nchi nzima na kwa kutumia vyanzo na teknojia mbalimbali ili kuhakikisha watanzania wengi wananufaika.