Raia wa Malawi wakamatwa Zanzibar kwa kuvunja Sheria za Uhamiaji

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:13 PM Aug 06 2025
Raia wa Malawi wakamatwa Zanzibar kwa kuvunja Sheria  za Uhamiaji
Picha: Rahma Suleiman
Raia wa Malawi wakamatwa Zanzibar kwa kuvunja Sheria za Uhamiaji

Raia watano kutoka nchini Malawi wamekamatwa katika Bandari ya Malindi, Zanzibar kwa kosa la kuingia nchini kinyume na taratibu za uhamiaji, huku wakieleza kuwa walikuja kufanya kazi za ndani bila kuwa na vibali halali.

Akizungumza na Nipashe Digital, Mrakibu wa Uhamiaji kutoka Kitengo cha Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Makao Makuu ya Uhamiaji Zanzibar, Hamdu Seif, amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Julai 31, 2025 walipowasili bandarini wakitokea Dar es Salaam.

Seif amebainisha kuwa mara baada ya kukamatwa, raia hao walipewa fursa ya kulipa faini kwa mujibu wa sheria, lakini walishindwa kutimiza masharti hayo na hivyo kufikishwa mahakamani.

“Walipohojiwa, walikiri kuwa walikuja Zanzibar kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, lakini hawakuwa na nyaraka yoyote ya uhamiaji inayowaruhusu kuingia au kufanya kazi nchini,” amesema Seif.

Watuhumiwa hao wameshtakiwa kwa kosa la kuwepo nchini kinyume na sheria, chini ya Kifungu cha 47(1)(i) cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54, mapitio ya mwaka 2023.

Mahakama imewataka kulipa faini ya Shilingi 500,000 kila mmoja, lakini walishindwa kulipa na hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza).