Ni mwaka usiokuwa na kushinda bila kupigiwa kura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:47 PM Aug 06 2025
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dk. Ramadhan Kailima
Picha: INEC
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dk. Ramadhan Kailima

TARATIBU, sheria na kanuni za uchaguzi mwaka huu, zimeondoa mazoea ya mgombea pekee kutangazwa mshindi bila kupigiwa kura na wananchi, na sasa atakuwa mbunge au diwani iwapo atapata kura nyingi za ndiyo dhidi au hapana kati ya kura halali zilizopigwa.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Dk. Ramadhan Kailima, anasema wakati akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu 2025, kwa wadau wa vyombo vya habari Dar es Salaam hivi karibuni.

"Kwa mujibu wa vifungu vya 54 na 66 vya sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani (2024), endapo kutakuwa na mgombea halali wa ubunge au udiwani, aliyeteuliwa, msimamizi atamtangaza kuwa mgombea pekee.

"Mgombea pekee wa nafasi hizo, atapigiwa kura ya ndiyo au hapana na atakuwa amechaguliwa kihalali kuwa mbunge au diwani ikiwa atapata kura nyingi za ndiyo, kati ya zote halali zilizopigwa". anasema Dk. Kailima.

Anaeleza, endapo atashindwa kupata idadi ya kura zinazohitajika, msimamizi wa uchaguzi ataitaarifu tume matokeo hayo, na utapangwa uteuzi mwingine wa ubunge au udiwani.

Baadhi ya wabunge waliopita bila kupingwa (2020) na majimbo yao kwenye mabano ni Hamis Kigwangalla (Nzega Vijijini), Nape Nnauye (Mtama), Vita Kawawa (Namtumbo) na January Makamba (Bumbuli).

Wengine ni Sagini Abdallah (Butiama), Alexander Mnyeti (Misungwi), Job Ndugai (Kongwa),  Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa), Taletale Shabani (Morogoro Mashariki) na Ahmed Shabiby (Gairo).

Baadhi ya wagombea ubunge watakaopigiwa na wananchi kura za ndiyo au hapa ni pamoja na mbunge wa zamani wa Bukombe Dk. Doto Biteko, Salma Kikwete (Mchinga) na Ridhiwani Kikwete (Chalinze).

KUMALIZA MALALAMIKO

Dk. Kailima anasema suala la kushughulikia malalamiko ya uchaguzi kutoka kwa wanaogombea urais, ubunge na udiwani, limepewa sura mpya baada ya kuundwa kamati za kushughulikia changamoto hizo na kutoa ufumbuzi.

Anazitaja kamati hizo zinazoundwa kuwa ni kamati ya maadili ya rufaa, kamati ya maadili ya taifa, kamati ya maadili ya jimbo na kamati ya maadili ya kata.

"Kamati hizo zitasimamia na kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni, kuanzia hatua ya kwanza hadi kukamilika muda wa kampeni. Tume inavisisitiza vyama vya siasa kuzitumia kamati kuwasilisha malalamiko wakati wote badala ya njia nyingine kama vyombo vya habari," anaongeza Dk. Kailima.

Akinukuu kipengele cha 5.15, cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani 2025, anasema kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi, 2024 ambaye na uamuzi wa kamati hizo za maadili, anaruhusiwa kwenda mahakamani.

Aidha, anawakumbusha wadau wa kamati za maadili ya uchaguzi kutekeleza wajibu wao kwa kutatua migogoro ili kusimamia na kuhakikisha kampeni zinafanyika kwa amani, haki na utulivu.

NAFASI YA MAWAKALA

Dk. Kailima anakumbusha vyama vya siasa kuteua mawakala na kufikisha majina yao INEC Oktoba 22 mwaka huu." Kifungu cha 77 cha Seria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2024, kinavitaka vyama vinavyoshiriki uchaguzi, baada ya kuteua wagombea, kuwasilisha majina ya mawakala wa kusimamia siku saba kabla ya uchaguzi. Kwa mwaka huu itakuwa ni Oktoba 22."

Anavikumbusha pia kuwasilisha barua ya utambulisho wa kila wakala na kituo alichopangiwa, picha zao. Na kama wakala hana picha, awasilishe moja ya vitambulisho kama kadi ya mpigakura, kadi ya NIDA, leseni ya udereva au pasipoti ya kusafiria.

Mkurugenzi huyo pia anavikumbusha vyama kuteua mawakala wengine ili inapotokea dharura, mwingine azibe nafasi na kuvikumbusha kuwa watakula kiapo cha kutunza siri mbele ya msimamizi wa uchaguzi Oktoba 22 mwaka huu

Akiwasilisha Mwongozo wa Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari Kuripoti Uchaguzi Mkuu wa 2025, Dk. Egbert Mkoko, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine anawakumbusha kujenga uelewa kwa wapigakura kuhusu sera, ajenda za kisiasa na kuwahamasisha wananchi kupiga kura.

“NI muhimu kutoa taarifa zinazochochea uwajibikaji wa kisiasa ili kudumisha amani na demokrasia katika kipindi chote cha uchaguzi kupitia taarifa sahihi ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi, anakumbusha,” Dk. Mkoko.

Anaongeza kuwa ni lazima kuzingatia sheria inayokataza kufanya kampeni kwa namna yoyote siku ya kupiga kura , ikiwamo kuvaaa mavazi yenye alama za chama au mgombea yeyote.

Anafafanua kuwa asubuhi siku ya Jumatano Oktoba 29, magazeti, redio, runinga na vyombo vyote vya mtandaoni visiripoti chochote kinachohusiana na kampeni au jambo lolote kuhusu masuala ya kukipigia kura chama au mgombea fulanii na picha zake, au video na sauti zake kwa sababu ni ukiukaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.

Dk. Mkoko anawahimiza wanahabari kutochapisha matokeo ya uchaguzi kabla ya kutangazwa rasmi na INEC na kujiepusha na kuingia kwenye vituo vya kupigia kura bila idhini na vibali vya tume.

Katika wosia wake kwa vyombo vya habari Mkurugenzi wa Habari wa Tume Huru ya Uchaguzi, Giveness Aswile, anasisitiza ulazima wa kutoa  taarifa ambazo zitamuacha  mwandishi, chombo chake na Tanzania salaam kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Hili lisiondoke kwenye mioyo yenu. Jiulize ninapotoa taarifa hizi, mimi, chombo changu na taifa tutabaki salama? Ni lazima tukumbuke Tanzania kwanza siyo kingine chochote,” anahimiza Giviness.

Anaongeza kuwa wakati wote wa kufanya kazi wanahabari wazingatie katiba ya nchi, sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi na kuwaelimisha wananchi kuzishikilia kwa kuwa msingi wa mafanikio ya uchaguzi na kubaki na taifa lenye amani ni kuzingatia sheria.

Kura yako Haki yako, Jitokeze Kupiga Kura