Raia Sri Lanka, Watanzania kizimbani madai kuingiza dawa zenye madhara

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:28 AM Aug 06 2025
Raia wawili wa Sri Lanka na Watanzania watano, wakiwa chini ya ulinzi wa askari polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusomewa mashtaka ya kuingiza zaidi ya tani 11 za vitu vyenye madhara
PICHA: IMANI NATHANIEL
Raia wawili wa Sri Lanka na Watanzania watano, wakiwa chini ya ulinzi wa askari polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusomewa mashtaka ya kuingiza zaidi ya tani 11 za vitu vyenye madhara

RAIA wawili wa Sri Lanka pamoja na Watanzania watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya kuingiza zaidi ya tani 11 za vitu vyenye madhara vinavyohusiana na dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa.

Raia wa Sri Lanka waliotajwa ni Jagath Wellalage (46), mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni, pamoja na Santhush Hewage (25), mfanyabiashara mkazi wa Masaki.

Watanzania walioshtakiwa pamoja nao ni: Riziki Shaweji (40), mfanyabiashara mkazi wa Masaki, Andrew Nyembe (34), wakala wa forodha na usafirishaji mkazi wa Gongo la Mboto, Mariam Ngatila (40), mfanyabiashara mkazi wa Masaki, Ramadhan Said (57), mfanyabiashara mkazi wa Kifuru, na Godwin Maffikiri (40), dereva mkazi wa Oysterbay.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga jana, Wakili wa Serikali Eric Davies, alidai kuwa shauri hilo jipya la uhujumu uchumi namba 19066/2025, linawahusisha washtakiwa hao kwa kosa moja la kuingiza dawa zenye madhara nchini.

Wakili Davies alidai kuwa mnamo Julai 15, 2025, washtakiwa walitenda kosa hilo katika Bandari Kavu ya Makontena ya Said Salim Bakhresa (SSB-ICD), iliyoKo eneo la Sokota, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.

Katika eneo hilo, walidaiwa kuingiza ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dawa aina ya Mitragyna speciosa, zenye uzito wa tani 11.596 kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa ni shtaka la uhujumu uchumi, ambalo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kulisikiliza bila kibali maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakili Davies alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, na kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana kisheria, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Hakimu Kiswaga alikubaliana na maombi hayo na akaahirisha shauri hilo hadi Agosti 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa, huku akiagiza kuwa mchakato wa kesi hiyo uendelee kwa njia ya mtandao, na washtakiwa wataendelea kuwa mahabusu hadi hapo upelelezi utakapokamilika au hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.