SERIKALI imesema uzalishaji wa Mahindi hapa nchini umeongezeka kutoka Tani milioni nane kwa msimu wa mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani milioni 12.26 kwa mwaka 2023/2024,huku ikisisitiza lengo la serikali ni kuhakikisha taifa linajilisha lenyewe na kulisha mataifa mengine.
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughilikia Maendeleo ya Mazao,Usalama wa Chakula na Ushirika,DK Stephen Nindi katika Mkutano wa wadau wa mahindi uliofanyika jana katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Dodoma.
DK Nindi alisema ongezeko hilo no.sawa na asilimia 53 huku akisema hayo yote hayo yanatokana na uwekezaji unaofanywa na serikali katika sekta ya Kilimo ndio maana uzalishaji unaongeza kila mwaka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
"Uzalishaji wa mahindi unaongezeka kila mwaka katika mikoa inayolima mahindi kwa wingi nawaaiaitiza wakulima endeleeni kulima kwa kufuata kanuni za kilimo,"alisema DK Nindi.
Aidha alisema anaipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA) kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha kila zao linapiga hatua kwenye uzalishaji.
Mbali na hilo alisema,takribani asilimia 80 ya wakulima wa zao la mahindi ni wakulima wadogo ambapo alisema serikali itaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuhakikisha kila mkulima analima kwa kufuata kanuni za kilimo kutoka kwa Maafisa Ugani.
Alisema serikali itaendelea kuboresha sekta ya kilimo katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanapiga hatua ikiwemo kunufaika na kilimo wanachofanya katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COPRA Irene Mlola alisema moja ya mikakati ya ya Mamlaka hiyo iliojiwekea ni kuwaleta pamoja wakulima wa mazao ya mahindi ili kuhakikisha kilimo hiko kinazidi kukua na kukidhi hitaji la solo katika maeneo mbalimbali.
Mlola alisema jukumu la serikali ni kuhakikisha inadhibiti nafaka na mazao mchanganyiko ili kihakikisha wakulima wanalima na kuvuna mazao bora lakini pia wanapeleka sokoni mazao yaliyo Bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa ubora wa mbegu nchini (TOSCI),Nyasebwa Chimagu alisema serikali imejipanga kwa kila kitu kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora ili waweze kuongeza uzalishaji.
Chimagu alisema wakulima wanapaswa kutumia mbegu bora ambazo zimesajiliwa na serikali3na si kutumia mbegu aina yoyote ile na kuongeza kuwa kilimo kinalipa hivyo wanapaswa kutumia mbegu Bora.
Chimagu alisema TOSCI itaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine ili kuhakikisha wakulima wote wanatumia mbegu Bora ili waweze kuongeza uzalishaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED