JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu, tuliangalia mikakati mbalimbali inayosaidia kuongeza idadi ya wanawake viongozi katika siasa.Tuliona nafasi ya jamii, wanawake wenyewe pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha mikakati hiyo inafanikiwa.
Katika safu yetu leo, tutaangalia faida na mabadiliko chanya yaliyopatikana katika maeneo ambayo wanawake wameshika uongozi wa kisiasa. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira.
Viongozi wanawake hufanikisha kupunguza vitendo vya rushwa, kupitia mazungumzo na wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa mitaa, vijiji na wananchi wa kawaida, mambo makubwa mawili, yamewekwa wazi. Mosi, katika maeneo ambayo wanawake wameshika madaraka ya kisiasa, yalitokea mabadiliko makubwa chanya katika kipindi cha uongozi wao. Pili, changamoto za kijamii ambazo awali hazikuwa zikipewa umuhimu, zilianza kuangaliwa kwa jicho jingine.
Je, kuna mabadiliko yoyote yameonekana katika maeneo ambayo wanawake wameshika uongozi wa kisiasa? Katika mazungumzo na viongozi hao, wanaeleza kuwa wamebaini mambo makubwa matatu.
Mosi, katika maeneo mengi ambayo wanawake wameshika madaraka ya kisiasa, wananchi wanakiri kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya wakati wa kipindi cha uongozi wao.
Pili, kumekuwa na msukumo wa kufuatilia, kuibua na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kijamii ambazo awali hazikuwa zikipewa umuhimu unaostahili.
Tatu, viongozi wa kisiasa wanawake wanatoa kipaumbele kwa mambo yanayogusa moja kwa moja au yanayoweza kuleta madhara kwa jamii nzima. Wanawake viongozi mara nyingi hutoa kipaumbele kwenye masuala yanayogusa jamii moja kwa moja ama yale ambayo yasiposhughulikiwa, yanaweza kuleta athari kubwa.
Miongoni mwa mabadiliko chanya yanayoonekana katika maeneo ambayo wanawake wameshika madaraka ya kisiasa, ni kupungua kwa kesi za rushwa. Pengine kwa sababu wanawake huelekea kuathirika moja kwa moja na huduma duni, wanapopata nafasi za uongozi wa kisiasa wanakuwa na motisha ya kweli ya kuhakikisha utawala bora na usimamizi mzuri wa fedha za umma.
Kadhalika inaelezwa kwamba katika maeneo ambayo yanaongozwa na wanawake, kesi za rushwa ni chache sana au hazipo. Kadhalika inaelezwa kuwa viongozi wanawake huwa na viwango vya chini vya kushiriki katika vitendo vya rushwa.
Kauli hii ina maana kubwa sana katika harakati za kushawishi kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake katika siasa. Kwa kuwa ushiriki wa wanawake katika uongozi hujenga uongozi wenye uwajibikaji zaidi na usiogubikwa na rushwa, ni vema jamii ikaliona hilo na kuwaunga mkono wake ili kuwa na idadi kubwa zaidi na hatimaye jamii yenye uwajibikaji wa hali ya juu.
Ipo mitazamo mbalimbali inayounga mkono dhana ya wanawake viongozi kuwa waadilifu zaidi. Kimalezi, wanawake kwa kawaida hupewa malezi ya kutilia mkazo maadili, uaminifu na uadilifu tangu wakiwa wadogo. Hii huwafanya kuwa waangalifu zaidi katika maamuzi yao ya kisiasa na kuepuka vitendo vya kifisadi.
Uangalizi mkali wa jamii, ni sababu nyingine inayowafanya wanawake waogope kabisa kujihusisha na masuala ya rushwa pindi wanapokuwa viongozi wa kisiasa. Hakuna asiyeelewa kwamba wanamke wanaposhika nafasi za uongozi huangaliwa kwa macho ya ukosoaji zaidi na jamii.
Hii huwafanya wajihadhari zaidi ili kuepuka kashfa zitakazoharibu sifa yao. Ingawa hoja hii haina ushahidi wa kisanyansi wa kuiunga mkono, lakini wanasiasa wengine hujitosa kuwania uongozi wa kisiasa ili kusaidia kutatua changamoto katika maeneo yao.
Katika mazungumzo na baadhi ya watia nia, inaonekana wengi huamua kuomba ridhaa ya kuongoza baada ya kuchoshwa na changamoto katika maeneo yao. Kiu ya kuleta mabadiliko, kubadili hali duni na kusaidia jamii zao, huwapa msukumo wa kuomba nafasi ya kuongoza.
Kwa hiyo wanapofanikiwa kuingia kwenye uongozi, lengo lao kubwa linakuwa kusaidia jamii, hasa katika masuala ya afya, elimu, na ustawi wa familia. Hii huwafanya kuwa na mtazamo wa huduma kuliko kujitajirisha binafsi kupitia rushwa.
Tafiti kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa zinaonesha kuongezeka kwa uwakilishi wa wanawake katika mabunge kunaweza kupunguza viwango vya rushwa. Takwimu zinadokeza kwamba nchi zenye kiwango kikubwa cha ushiriki wa wanawake katika siasa huwa na viwango vya chini vya rushwa.
Kadhalika zipo ripoti zinazobainisha kuwa wanawake wengi viongozi wana mwelekeo wa uwajibikaji zaidi, hasa katika uwazi wa matumizi ya rasilimali za umma na kwamba wananchi huwaamini wanawake zaidi katika uongozi wa umma ikilinganishwa na wanaume, hasa katika masuala ya fedha na maamuzi ya kiutawala.
Inabainishwa zaidi kuwa katika nchi ambazo wanawake wamepewa nafasi zaidi katika uongozi wa kisiasa na kiutendaji, viwango vya kuripoti rushwa hupungua, ikimaanisha uwepo wao huongeza uadilifu wa mifumo.
Taasisi ya Transparency International katika baadhi ya ripoti zake inaonesha kuwa wanawake huonekana kama viongozi waaminifu zaidi, na mara nyingi wanakuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa.
Ingawa si sahihi kusema kwamba wanawake wote hawahusiki na rushwa, ushahidi wa kitaaluma na uzoefu wa nchi mbalimbali unaonesha kuwa wanawake wanasiasa huwa na uwezekano mdogo wa kujihusisha na rushwa ukilinganisha na wanaume.
Kwa hali hiyo, kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa si tu ni hatua ya kuimarisha usawa wa kijinsia, bali pia ni mkakati mzuri wa kupunguza rushwa katika jamii.
Kwa kuzingatia maelezo hayo, ni wazi kuwa ongezeko la wanawake katika nafasi za uongozi huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya rushwa. Wanawake wengi huonesha maadili ya juu, uwajibikaji, na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao, hali inayosaidia kuimarisha mifumo ya utawala bora.
Kwa msingi huu, jamii kwa ujumla, vyama vya siasa, taasisi za serikali na mashirika ya kiraia wanapaswa kuchukua hatua madhubuti za kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi. Hii ni pamoja na kutoa nafasi sawa za kugombea, kuwajengea uwezo wa kiuongozi, na kuondoa vikwazo vya kijamii na kiutamaduni vinavyowazuia wanawake wengi kufikia nafasi hizo.
Kuwapa wanawake nafasi zaidi katika uongozi si tu ni suala la usawa wa kijinsia, bali ni mkakati wa msingi wa kupambana na rushwa na kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Swali la kufikirisha:
Ni mabadiliko yapi yameonekana katika maeneo ambayo wanawake wameshika uongozi wa kisiasa?
Tuandikie maoni yako kupitia:
Instagram: Joyce_bazira
Simu: 0784 358262
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED