JULAI 27, mwaka huu, Israel inatangaza kusitishwa kwa mashambulizi huko ukanda wa Gaza, lakini Umoja wa Mataifa (UN), unasema licha ya tangazo hilo vita vipo pale pale.
Umoja wa Mataifa (UN), unasema licha ya tangazo hilo vita vipo pale pale. UN inasema kuendeleza kwa mapigano, kumesababisha takribani Wapalestina 1,400 kuuawa wakitafuta chakula na kuongeza:
“Vikosi vya Israel vimeendelea kushambulia maeneo ya njia za misafara ya chakula na karibu na vituo vya misaada vya Gaza Humanitarian Foundation (GHF),” inasema Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Palestina (OHCHR).
Hata hivyo mfumo wa kudondosha chakula kutoka kwenye ndege angani, unatajwa kuwa ni ghali zaidi kuliko kutumia malori na kusambaza wa misaada kwa njia ya anga hugharimu angalau mara 100 zaidi ya matumizi ya malori ambayo yanabeba msaada mara mbili zaidi ya ndege.
“Usambazaji wa angani ni gharama kubwa usiotosheleza na usio na ufanisi,” tovuti ya UN inafafanua na kwamba Kati ya Julai 30 na 31, mwaka huu pekee, Wapalestina 105 waliuawa na wengine 680 kujeruhiwa katika njia za misafara ya misaada katika eneo la Zikim, Kaskazini mwa Gaza, kusini mwa Khan Youni na karibu na vituo vya GHF katikati mwa Gaza na Rafah, kwa mujibu OHCHR, Ijumaa, wiki iliyopita.”
Umoja wa Mataifa, unasema, tangu Mei, Wapalestina 1,373 wameuawa walipokuwa wakitafuta chakula; 859 wakiwa karibu na vituo vya GHF na 514 wakiwa katika njia za misafara ya chakula.
OHCHR imeeleza kuwa wengi wanadaiwa waliuawa na Jeshi la Israel na ingawa wanatambua uwepo wa makundi mengine yenye silaha katika maeneo hayo, hawana ushahidi unaoonesha ushiriki wao katika mauaji hayo.
“Ofisi haina taarifa kuwa wapalestina waliouawa walikuwa wakishiriki moja kwa moja katika mapigano au walikuwa tishio kwa vikosi vya usalama vya Israel au watu wengine.
“Kila mtu aliyeuawa au kujeruhiwa alikuwa akihangaika kuokoa maisha yake, na ya familia na wategemezi wao,” taarifa hiyo ilisema shirika hilo.
SHERIA KIMATAIFA
Ofisi hiyo inasisitiza kuwa kulenga kwa makusudi raia wasiokuwa sehemu ya mapigano na kutumia njaa kama mbinu ya vita kwa kuzuia vitu muhimu vya kuendeleza maisha, ikiwamo kuzuia misaada kwa makusudi, ni uhalifu wa kivita.
“Iwapo vitendo hivi ni sehemu ya mashambulizi ya kimfumo au ya kiwango kikubwa dhidi ya raia, vinaweza pia kuhesabiwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu,” OHCHR inaongeza, ikisisitiza madhara ya mkusanyiko wa matukio haya na vizuizi vya misaada ya kibinadamu.
“Kila tukio la mauaji lazima lichunguzwe kwa haraka na kwa uhuru, na wote waliohusika wawajibishwe. Hatua za haraka zichukuliwe ili kuzuia kurudiwa kwa matukio haya,” inasema.
ALIYEKUMBWA NA NJAA
"Watoto wangu wote wanne wanalia kwasababu hawajakula chakula kwa siku nne," anasema baba mmoja wa Gaza. Nilikwenda katika kituo kinachotoa chakula cha misaada nikiwa na matumaini ya kupeleka nyumbani angalau mfuko mmoja wa unga. Lakini nilipofika hapo, sikujua la kufanya," anaiambia BBC Idhaa ya Kiarabu.
"Nisaidie kuwaokoa waliojeruhiwa, nisaidie kuondoe miili ya waliouawa, au nitafute mfuko wa unga? Niko radhi kufa kupata mfuko mmoja wa unga, ili watoto wangu wapate kula."
Inaelezwa pia, utapiamlo, njaa na mauaji karibu na maeneo ya kutoa misaada yamezidi huko Gaza, kwa kuwa watu wanategemea msaada unaosambazwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani na Israel (GHF).
"Zaidi ya Wapalestina 1,000 sasa wameuawa na Jeshi la Israel wakijaribu kutafuta chakula huko Gaza GHF, ilipoanza shughuli zake Mei," anasema Thameen Al-Kheetan, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
"Kufikia Julai, tumerekodi vifo vya 1,054 vya watu waliouawa huko Gaza walipokuwa wakijaribu kupata chakula; 766 kati yao waliuawa karibu na maeneo ya GHF na 288 karibu na misafara ya misaada ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kibinadamu," anasema.
ONGEZEKO LA VIFO
Shirika la GHF lilianza shughuli zake Gaza mwishoni mwa Mei, mwaka huu, ikisambaza misaada michache kutoka maeneo kadhaa ya kusini na kati ya Gaza.
Hatua hiyo ni baada ya Israel kuzuia msaada wowote kuingia Gaza kwa takribani wiki 11, Dk. Mohammed Abu Salmiya, Mkurugenzi wa Hospitali ya Shifa Gaza, anasema watoto 21 wamekufa kwa utapiamlo na njaa katika eneo hilo kwa saa 72 zilizopita.
Watoto 900,000 huko Gaza wanakabiliwa na njaa na 70,000 kati yao wana utapiamlo, anaiambia BBC na kuongeza kuwa wanakabiliwa na tishio la kufa, daktari anaonya na wagonjwa wa kisukari na figo pia wako hatarini.
Msemaji wa Wizara ya Afya, inayoongozwa na Hamas, anasema watu 33 wakiwamo watoto 12 wamefariki katika muda wa saa 48 zilizopita na vifo kutokana na utapiamlo vinafikia 101, ambapo 80 ni watoto, tangu kuanza kwa vita mwaka 2023, imebainishwa.
Shirika la Chakula Duniani (WFP), linasema wakazi wote wa Gaza wanakabiliwa na njaa na utapiamlo umekithiri huko kina mama na watoto 90,000 wakihitaji matibabu ya dharura.
Takribani mtu mmoja kati ya watatu, anakosa kula kwa siku kadhaa, WFP imesema katika taarifa siku ya mwishoni mwa wiki na kwamba msaada wa chakula ndiyo njia pekee itakayowasaidia wakazi hawa, kwani gharama ya mfuko wa kilo moja ya unga imepanda hadi zaidi ya dola 100 katika masoko ya ndani.
Machi, mwaka huu, Israel ilifunga vivuko vyote kuelekea Gaza na kuzuia bidhaa zote, ikiwa ni pamoja na chakula, mafuta na madawa kuingia na ilianza tena mashambulizi yake ya kijeshi wiki mbili baadaye na kuhitimisha usitishaji mapigano wa miezi miwili na Hamas.
Vizuizi hivyo pia vimekata dawa muhimu, chanjo na vifaa vya matibabu vinavyohitajika na mfumo wa afya uliozidiwa wa Gaza na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ina hivi karibuni kwamba, malori 4,400 ya misaada ya kibinadamu zimeingia Gaza kutoka Israel tangu katikati ya Mei.
Mizigo mingine 700 ya malori ilikuwa ikisubiri kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa, kutoka upande wa Gaza wa maeneo yake ya vivuko, inaongeza taarifa hiyo.
UN/BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED